Polisi nchini Kenya wamerusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa upinzani National Super Alliance ambao wamekuwa wakiandamana mjini Kisumu, magharibi mwa nchi hiyo.
Maandamano pia yamefanyika katika miji mingine mikuu ingawa hali imekuwa tulivu.
Mwandishi wa BBC David Wafula anasema maandamano ya leo jijini Nairobi, ukilinganisha na maandamano ya awali, yalikuwa na utulivu zaidi na idadi ya waliojitokeza walikuwa wengi.
Muungano wa Nasa umekuwa ukifanya maandamano kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza mageuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya.
Uchaguzi ambao umepangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba umeingiwa na utata baada ya mgombea wa Nasa Raila Odinga kutangaza kujiondoa rasmi Jumanne.
Mapema leo, Mahakama Kuu pia iliagiza mgombea wa Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot ajumuishwe kwenye uchaguzi huo.
Muungano wa Nasa unataka uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku 90 na wagombea wateuliwe upya.
Huyu alijitokeza na mbwa kuandamana
Kando na maandamano mijini, Nasa wameandaa pia mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Uhuru Park katikati mwa jiji la Nairobi.
Shirika la habari la AFP linasema waandamanaji mjini Kisumu, ambayo ni ngome ya upinzani, wamekuwa wakichoma matairi kwenye barabara.
Mahakama yafutilia mbali ushindi wa Kenyatta
Baadhi wameonekana kwenye picha wakiwa na manati ambazo mara kwa mara wamezitumia kuwarushia polisi mawe.
Bw Odinga aliwahimiza wafuasi wake kuendelea kuandamana kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi IEBC ambayo inatarajiwa kutangaza msimamo wake baada ya kujiondoa kwa mgombea huyo wa Nasa wakati wowote.