RAIS Yoweri Museveni wa Uganda ametekeleza ahadi aliyoiweka Agosti 5, mwaka huu kwa Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi bandari ya Chongoleani, jijini Tanga, Tanzania
Wakati wa uzinduzi huo, Rais Magufuli alimuomba Rais Museveni wataalamu waliogundua mafuta katika Ziwa Abert nchini Uganda kushirikiana na wataalamu wa Tanzania katika utafiti wa mafuta katika Ziwa Tanganyika na Eyasi nchini. “Rais Museveni wa Uganda alitumia wataalamu wake ambao aliwapeleka kusoma na kisha kufanya utafiti huo na hatimaye kugundua mafuta.
Kwa maana hiyo, Tanzania tutawatumia hawa watalaamu wa Uganda katika kufanya utafiti wa mafuta Ziwa Tanganyika na Eyasi,” alisema Rais Magufuli siku hiyo. Takwimu za awali zinaonesha kwamba maeneo hayo yana kiwango kikubwa cha mafuta. Katika mkutano huo, Rais Museveni wakati akizungumza alionesha nia ya kuileta timu hiyo Tanzania huku naye akitaka gesi asili kufikishwa Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, timu hiyo ya wataalamu ambayo ilifika nchini jana na kufanya mazungumzo wizarani hapo, sasa inaelekea Ziwa Eyasi kwa siku mbili kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo zaidi. Kufika kwa timu hiyo ya watu sita ikiongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini Uganda, Robert Kasande kunaamsha upya mchakato wa kutafuta mafuta katika Ziwa Tanganyika na Eyasi, ambako tayari kuna utafiti kadhaa zimeshafanywa kuanzia miaka ya 1950.
“Tumefika hapa na tupo tayari kubadilishana uzoefu ambapo utalenga katika kuangalia tafiti zilizowahi kufanyika nyuma, kutembelea maeneo husika na kuweka mikakati ya namna bora ya kufanya utafiti kwa ubora wa hali ya juu kwa kushirikiana na Tanzania,” alisema Kasande. Katika kikao hicho cha utambulisho kilichoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, walikuwepo pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo na wataalamu kutoka Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).
Rais Magufuli amekuwa katika harakati za kutaka kuhakikisha kuwa rasilimali ya mafuta inagunduliwa na kuanza kuleta manufaa kwa wananchi. Dk Kalemani akizungumza katika kikao hicho, alisema; “Sisi kama Tanzania tupo tayari kubadilishana uzoefu na wataalamu wa Uganda kwenye utafiti wa mafuta na kuanza kazi mara moja; hata hivyo pia tupo tayari kubadilishana nao uzoefu kwenye masuala ya gesi kwa kuwa tuna utaalamu huo, lengo likiwa ni kuimarisha sekta hizi za mafuta na gesi kwa nchi zote mbili.”
Ameongeza kwa kuwa Tanzania ina uzoefu mkubwa kwenye utafiti wa gesi asilia, wapo tayari kutuma wataalamu nchini Uganda kushirikiana kwenye utafiti wa gesi nchini Uganda. ZIWA EYASI Hili ni ziwa la magadi ambalo mito yake huishia katika ziwa hilo. Kijiografia ziwa hilo lipo kwenye ukanda wa Bonde la Ufa upande wa mashariki chini ya beseni la Serengeti, Kusini mwa Hifadhi ya Serengeti na kusini magharibi mwa Kreta ya Ngorongoro.
Mito mikubwa inayoingia maji katika ziwa hili ni mto Sibiti na Mto Baray. Maeneo haya ni nyumbani kwa makabila ya Datooga na Hadzabe na eneo maarufu la korongo. Ziwa hili lipo magharibi mwa Ziwa Manyara kiasi cha kilometa 155 magharibi mwa Arusha likiwa na ukubwa wa maili za mraba 400 sawa na kilometa za mraba 1,050. Katika historia takribani miaka mitatu iliyopita, Tanzania ilifanya mazungumzo na kampuni za Total na BP ya kutafuta mafuta katika ziwa hilo.
Kampuni nyingine zinazotafuta mafuta nchini kutoka Norway ni Statoil, Kampuni ya Brazil ya Petrobras, Kampuni ya Uholanzi ya Shell, BG Group na Exxon Mobil. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Profesa Sospeter Muhongo alisema Total wameonesha nia ya kutafuta mafuta katika Ziwa Eyasi na hivyo kuongeza ushindani. Mei 2015, kampuni ya China ya usakaji mafuta ya CNOOC Ltd na kampuni ya gesi ya Urusi ya Gazprom pia ziliwasilisha zabuni za vitalu vinne kati ya nane vilivyopo.
UTAFITI WA ANGA Aidha, Novemba 2015 dalili za kuwapo kwa mafuta zilikuwa dhahiri kwa Mkoa wa Arusha baada ya TPDC kufanya utafiti wa anga katika maeneo ya Ziwa Eyasi na Natron. Utafiti huo umeshafanyika mara mbili ambapo mara ya pili ulifanyika katika eneo la Eyasi Wembere na Mandawa eneo ambalo wataalamu wa Uganda watakwenda kulichungulia. Utafiti huo ulikamilika katikati ya Januari 2016 kwa gharama ya Sh bilioni 14 zikiwa ni fedha za Serikali ya Tanzania.
Kupatikana kwa mafuta nchini Kenya na Uganda katika ukanda wa Bonde la Ufa, unafanya kuwepo na imani kubwa kwamba Ziwa Eyasi litakuwa na nafasi ya kuwa na mafuta pia. Upimaji wa eneo hilo kwa kutumia ndege maalumu ulifanyika katika umbali wa kilomita 23,000. Utafiti huo ulifanywa huku ndege hiyo ikiwa katika umbali wa meta 80 hadi 100 kutoka usawa wa bahari katika spidi ya kilometa 220 kwa saa.
ZIWA TANGANYIKA Katika Ziwa Tanganyika, Kampuni ya Beach Energy ilishasema kwamba ziwa hilo lina uwezekano mkubwa wa kuwa na mafuta. Hata hivyo, eneo ambalo lilionekana dhahiri ni eneo la nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Hata hivyo, Beach Energy wamesema kwamba upo uwezekano mkubwa wa ziwa hilo kuwa na mafuta kiasi cha mapipa kadri ya milioni 200.
Taarifa hizi za kuwepo kwa mafuta ni za zamani hata kabla ya mafuta ya Ziwa Albert kuonekana katika miaka ya 2000 hivyo inakuwa ni kitu kipya kuanza kuthibitisha uwapo wa mafuta katika maeneo hayo. Mwaka 2008, DRC na Tanzania ilitiliana saini mkataba wa kufanya uchunguzi kwa pamoja, lakini kwa mujibu wa taarifa katika mitandao, mkataba huo haukutekelezwa. Maeneo ya DRC uwepo wa mafuta unaonekana kutokana na mafuta hayo kujitokeza wazi.