Rais wa Wakurdi nchini Iraq Massoud Barzani amejiuzulu kufuatia mgogoro kati ya Wakurdi na utawala wa Iraq wa jimbo hilo kutaka kujitenga na kuwa huru.
Rais Massoud Barzani ameachia wadhifa huo wakati eneo hilo linapambana na serikali kufuatia uhuru wake.
Kupitia barua iliyosomwa kwa bunge la Kurdi, Bw. Barzani amesema kuwa hataomba kuongezwa muhula baada ya huu alionao ukiwa unatarajiwa kukamilika siku nne zinazokuja.
"Ninaomba bunge kukutana ili kujaza nafasi hiyo," alisema
Wakurdi walipiga kura mwezi uliopita kuitenga Kurdistan lakini Iraq inasema kuwa kura hiyo ilikuwa kinyume na sheria, kisha jeshi la Iraq likaanzisha oparesheni ya kuukomboa mji uliokuwa chini ya wakurdi wa Kirkuk na kuteka vituo vya mafuta vya mji huo.
Bwana Barzani amesema atasalia kuwa mpiganaji wa kurdi na atazidi kutetea mafanikio ya watu wa Kurdistan.
Bw Barzani aliingia ofisini mwaka 2005 baada ya kuhusika katika wajibu mkubwa wa kuunda eneo huru la Kurdistan lililo kaskazini mwa Iraq baada ya Saddam Hussen kuondolewa madarakani.