Rais Uhuru Kenyatta amesema atatia saini kuwa sheria miswada ya sheria ya uchaguzi mara itakaporidhiwa na Bunge.
Akiwahutubia wananchi katika kituo cha mabasi cha Kaloleni katika kaunti ya Kilifi jana Rais Kenyatta amesema haoni tatizo lolote kuhusu miswada hiyo kwa sababu masuala yaliyoibuliwa na wapinzani yamezingatiwa pia.
Kenyatta ametoa kauli hiyo wakati Bunge lenye wabunge wengi wa chama cha Jubilee linahaha kukamilisha mchakato wa kujadili miswada miwili na kuipitisha kabla ya siku ya mwisho ya kufanya hivyo Alhamisi.
Mabunge yote mawili yaani Bunge la Taifa na Seneti yanajadili miswada inayolenga Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, na Sheria ya Uchaguzi na Makosa ya Uchaguzi kuelekea uchaguzi wa marudio.
Hata hivyo wabunge wa Nasa wamekataa kushiriki mjadala wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yaliyowasilishwa katika vikao vya Bunge la Taifa na Baraza la Seneti. Wabunge hao walisisitiza pia kwamba kiongozi wao Raila Odinga hatashiriki uchaguzi huo.
Uamuzi wa kutoshiriki mjadala huo ulifikiwa Jumatano iliyopita katika vikao vya wabunge wa Nasa.
Kiongozi wa wachache bungeni katika Bunge la Taifa, Mbunge wa Suba Kusini John Mbadi alisema hatua yao ya kutoshiriki mjadala huo imelenga kukwepa kuhalalisha “mchakato uliokosewa.”
“Baada ya kupitia miswada yote miwili, tumejiridhisha kwamba ni miswada hatari. Miswada hii haiku kikatiba na iko katika msingi uliokosewa kwa maudhui yake na mchakato mzima,” alisema Mbadi.
Akipinga miswada miwili kujadiliwa kwa pamoja na mabunge mawili, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr alisema, “Hatutashiriki katika uchaguzi ambao Jubilee wanatoka jasho kubadili magoli. Tunataka kuwaambia Jubilee hatutaruhusu hilo kutokea.”
Lakini Rais Kenyatta ameweka msimamo akisema; "Binafsi sioni tatizo lolote katika sheria hii na ikiwa Bunge litapitisha (miswada), nitatia saini, sina tatizo nayo kwa sababu imebeba mambo yaliyoibuliwa na upande wa upinzani.”
Rais, ambaye aliongozana na Makamu wake William Ruto amesema wako tayari kushiriki uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais Oktoba 26.
Kenyatta alisema mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani (Nasa), Raila Odinga anajishughulisha na mipango ya kutaka kuhakikisha uchaguzi huo unafutwa jambo alilosema halitatokea kama anavyotaka.
Soma: Mbunge ataka mahakama imzuie Raila kususia uchaguzi
"Sisi tunahaha kutafuta kura na leo tuko Kaloleni wakati yeye ameamua kuitisha mkutano na waandishi wa habari,” amesema.
"Kwa nini hayuko tayari tena kwenda kwenye sanduku la kura baada ya hukumu ya Mahakama ya Juu, ikiwa ana uhakika aliibiwa uchaguzi? Ikiwa hatashiriki uchaguzi huu basi sisi tutaendelea kuwatumikia wananchi,” amesema.
Katika mwendelezo wa kampeni zake, Rais amesema ukanda wa pwani kwamwe hauwezi kutengwa kimaendeleo.
"Nafahamu kwamba hata mtu aliyepigia upande wa upinzani ni Mkenya, ambaye anataka Rais anayewajibika. Nitatimiza hayo na miradi yote iliyoanzishwa na utawala wangu haitatelekezwa,” amesema.
Rais Kenyatta Kutia Saini Miswada ya Sheria Itakaporipotiwa na Bunge
0
October 11, 2017
Tags