Serikali Yawatengea Bilioni 531 Wafanyakazi Waliopandishwa Daraja

Serikali Yawatngea Bilioni 531 Wafanyakazi Waliopandishwa Daraja
Serikali imetenga Sh531 bilioni kwa ajili ya wafanyakazi waliopandishwa madaraja ambao taarifa zao zimehakikiwa na hazina utata.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas alisema kwa sasa Serikali imemaliza mchakato wa awali wa kusafisha watendaji hewa kwenye mfumo na wale ambao wataonekana kuwa ni halali mchakato wa kupandisha madaraja utaanza.

Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza na kufanyia kazi agizo la kupandisha wafanyakazi madaraja na katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha Serikali imetenga Sh487.7 bilioni kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi baada ya kuanza kwa mfumo mpya na kuondoa wafanyakazi wenye utata.

“Mchakato wa kupandisha madaraja unaendelea na wengine ambao hakuna mchakato mrefu kuwapandisha madaraja wamekwishapandishwa na wamelipwa na tayari katika robo hii Sh531 milioni zimeshalipwa kwa waliopanda katika ngazi zisizo na utata,” alisema.

Dk Abbas alisema Serikali imetenga Sh35.2 bilioni kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi huku Sh70.4 bilioni zikilipwa kwa ajili ya madai ya wafanyakazi sehemu kubwa ikiwa ni madai yasiyo ya mishahara kwa mwaka 2016/17 katika robo hii ya kwanza.

Awali mkurugenzi huyo alikanusha taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) kuhusu kauli ya Rais John Magufuli kutopandisha mishahara kwa wafanyakazi na Dk Abbas alisema kauli hiyo ililenga posho za madiwani na si wafanyakazi wote.

“Si kweli kuwa kauli ilijikita kwa wafanyakazi wa umma bali ni madiwani waliotaka kuongezewa posho kutoka Sh350,000 hadi 800,000 na si wafanyakazi na sisi kama Serikali tutawachukulia hatua walioeneza taarifa hii ya uongo,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad