Sheik Ponda Akanusha Tuhuma za Kutoa Maneno ya Uchochezi

Sheik  Ponda Akanusha Tuhuma za Kutoa Maneno ya Uchochezi
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amekanusha tuhuma kuwa alitoa maneno ya uchochezi alipozungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita.

Badala yake, Ponda amesema alitoa tahadhari kwa matukio yanayojitokeza na jinsi ya kuyakabili kwa mustakabali wa amani ya nchi.

Sheikh Ponda alishikiliwa na polisi kwa takriban siku mbili baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu safari yake ya Nairobi, Kenya alikokwenda kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika mkutano huo alizungumzia utekaji, kuokotwa kwa miili ya watu na mazungumzo aliyofanya na Lissu

Polisi walimhoji na kupekua nyumbani kwake wakituhumu kuwa alitoa maneno ya uchochezi.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kuripoti polisi, Sheikh Ponda alisema: “Nilizungumza kwa nia nzuri kwa masilahi ya Taifa na umma. Nilikuwa nakumbushia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwamba vina wajibu wa kusimamia amani na usalama.

“Kile nilichozungumza nimewaeleza nilikuwa sahihi na sikuwa na nia mbaya hata kidogo. Leo (jana) saa 3:00 asubuhi nimeripoti na nimeelezwa niondoke na watakaponihitaji muda wowote watanipigia simu.”

Kuhusu upekuzi uliofanyika nyumbani kwake Ubungo - Kibangu, Sheikh Ponda alisema hawakukuta chochote.

“Walidai wanatafuta kama kuna nyaraka zozote za uchochezi, lakini hawakuzikuta. Tuliporudi polisi dhamana ilishindikana kwa kuwa wakubwa hawakuwepo.”

Sheikh Ponda, mwanaharakati wa haki za Waislamu, alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi Oktoba 13 asubuhi kwa wito wa kamanda wa Jeshi la Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam ambaye alimpa saa 72 kufanya hivyo.

Baada ya kujisalimisha alishikiliwa kwa mahojiano na baadaye askari walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake na aliachiwa Oktoba 14 akitakiwa kuripoti jana.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Huyu Ponda anayejiita mwanaharakati wa haki za kiislam ni shetani mkubwa. Nia yake ni kufitinisha umna. Huyo Lisu aliemfuata huko Nairobi ni muislamu? Siasa ndio iliyompeleka Nairobi sio uislamu. Ponda alikuwa wapi wakati watu wanauwawa kule kibiti? Pengine yeye mwenyewe Ponda ni miongoni mwa muhusika wa ugaidi wa vile vitendo vya mauaji kule kibiti. Kupiga siasa kwa kisingizio cha imani za dini ni unafiki uliokithiri. Hata hiyo mitihani inayompata Ponda mara jela mara ndani mara polisi mara kupigwa ni moja kati ya adhabu na laana anayoipata kutoka kwa Mungu kutokana na unafiki wake. Kazi za kiroho kwa watumishi wa Mungu awe muislamu au mkiristo ni kubwa mno wala haiwezi kumpa nafasi mtumishi wa kweli wa Mungu kuhangaikia masuala ya siasa. Kazi za kuwahimiza waumini wa dini fulani kufuata na kutii makatazo ya mafundisho ya dini zao ili wawe raia wema duniani na akhera bado haijafanyika Tanzania na ushahidi ni jinsi gani vitendo vya kihalifu wa kutisha unavyoongezeka siku hadi siku . Ukimuona kiongozi wa dini anailaumu serikali kwa kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu katika jamii ambae yeye mwenyewe anaishi basi ujue huyo sio kiongozi wa dini. Kiuhalisia Serikali inatakiwa kuwalaumu viongozi wa dini ikiwa vitendo vya kihalifu vinakithiri katika jamii. Kazi kubwa ya serikali ni kusimamia sheria kwa wananchi wake ili waishi kwa amani na salama. Na usimamizi huo wa sheria kwa serikali kwa wananchi wake unakuwa rasisi kama jamani wanaiongoza imepikwa vizuri kimaadili kutoka kwa wazazi na viongozi wa dini. Sio kila kitu lawama kwa serikali na ndio maana wakati mwengine serikali inabidi inyooshe mkono wake wa vyombo vya sheria ndani ya jamii jambo ambalo mara nyingi huleta taswira ya vitisho katika jamii lakini ukweli ni kwamba katika jamii tulivu na yenye kufuata sheria polisi wa kazi gani?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad