Hilo limebainishwa na msemaji wa klabu hiyo Haji Manara wakati akiongea na waandishi wa habari leo kwenye makao makuu ya klabu ambapo amesema nakala za barua hiyo wamezipeleka TFF, Bodi ya ligi TPLB pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.
“Tumeliandikia barua shirikisho tukieleza dhuruma tunayofanyiwa na waamuzi pia nakala nyingine tumetuma kwa waziri mwenye dhamana ya michezo kwasababu haturidhishwi na maamuzi kwenye mechi zetu”, amesema Manara.
Manara ameeleza matukio mbalimbali ambayo klabu yake inalalamika kuhujumiwa ikiwemo Penalti mbili walizonyimwa dhidi ya Mbao FC ambapo mshambuliaji John Bocco alichezewa rafu lakini mwamuzi hakuchukua hatua sitahiki.
Matukio mengine ambayo Manara ameonesha kuchukizwa nayo ni kunyimwa Penalti kwenye mchezo dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita ambapo mlinzi Kelvin Yondani aliudaka mpira wa adhabu ndogo lakini mwamuzi Elly Saasi hakutoa adhabu ya Penalti.
Kwa upande mwingine Manara amesema klabu ya Simba inaendelea na maandalizi ya mchezo wake wa ligi dhidi ya Mbeya City chini ya kocha mkuu Joseph Omog na msaidizi wake Juma Masoud. Mchezo huo utapigwa siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.