Siri na Mipango ya Mauaji ya Bilioni Msuya Kujulikana Kesho

Siri na Mipango ya Mauaji ya Bilioni Msuya Kujulikana Kesho
Siri na mipango ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya na namna yalivyotekelezwa, zitaendelea kuanikwa kesho Jumatatu wakati kesi ya mauaji hayo itakapoendelea kusikilizwa.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wananchi wengi wa miji ya Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Bomang’ombe, inasikilizwa katika mahakama kuu kanda ya Moshi.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa,  aliuawa kwa kufyatuliwa risasi 22 za bunduki aina ya SMG ambapo 12 ndizo zilizompata risasi na kusababisha kifo chake.

Tukio hilo la aina yake, lilitekelezwa Agosti 7,2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai na watu wasiojulikana lakini polisi inawatuhumu watuhumiwa saba kuhusika na mauaji hayo.

Kesi hiyo ilisimama kusikilizwa Machi 21 mwaka huu, baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga uamuzi mdogo wa Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo.

 Awali kabla ya kusitishwa kwa usikilizaji wa kesi hiyo, kuliibuka mabishano ya kisheria kati yamawakili wa utetezi na mawakili waandamizi wa Serikali wanaoendesha kesi hiyo.

 Mabishano hayo yalitokana na hatua ya shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu kutoa ushahidi wa mdomo wa kukiri kosa wa mshitakiwa wa tatu, Ally Mussa Majeshi bila kuwasilisha maelezo yake.

Mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Lundu, walipinga utaratibu huo, wakisema ni kinyume cha sheria kwa vile maelezo hayo hayajapokelewa mahakamani.

 Jaji alikubaliana na hoja ya mawakili wa utetezi na kuzuia ushahidi huo, hali ambayo iliwasukuma mawakili wa Serikali wakiongozwa na Abdalah Chavula kuwasilisha notisi ya kukata rufaa.

Kesi hiyo sasa imepangwa kuendelea kusikilizwa kuanzia Oktoba 16 hadi Novemba 16 baada ya jopo la majaji wa mahakama ya rufaa iliyoketi Jijini Arusha kuitupa rufaa ya upande wa Jamhuri.

Ratiba iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Benard Mpepo, inaonyesha mashahidi 37 wa upande wa Jamhuri wataendelea kutoa ushahidi wao kutimiza idadi ya mashahidi 46.

 Washitakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne au Mredii, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed au Msudani au Mnubi na Ally Mussa au Mjeshi.

Wakati kesi ya Bilionea huyo ikiendelea kesho , mkewe Miriam Elisaria Msuya naye anasota mahabusu Jijini Dar Es Salaam kwa tuhuma za kumuua dada wa bilionea huyo aitwaye, Aneth Msuya.

Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana Mei 25,2016 katika eneo la Kibada Kigamboni Jijini Dar Es Salaam, mauaji ambayo yaliibua hisia na simanzi kubwa kwa familia ya bilionea huyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad