Siri ya Profesa Kitila Kun'goka ACT-Wazalendo

Siri ya Profesa Kitila Kun'goka ACT-Wazalendo
Wakati Profesa Kitila Mkumbo akitangaza kung’atuka rasmi uanachama wa ACT-Wazalendo siri kubwa imefichuka kuhusu hatua yake hiyo.

Hata hivyo, mwenyewe anasema kuwa sababu za yeye kufanya hivyo ameziweka wazi na kwamba anayetaka kusema lolote aseme.

Juzi, barua iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha imesainiwa na Profesa Kitila, ikiandikwa kwenda kwa Dorothy Semu, Kaimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo ilimnukuu ikisema kuwa ameamua kung’atuka kwa hiyari yake.

Kwa mujibu wa barua hiyo, Profesa Kitila ilisema, “Utakumbuka kuwa nilipoteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara katika Serikali ya CCM nilijiuzulu nafasi yangu ya ushauri wa chama na tukakubaliana kuwa ningeendelea kuwa mwanachama wa kawaida.”

Hata hivyo, Profesa Kitila alisema uzoefu wa miezi sita wa kutumikia nafasi yake serikalini umeonyesha ni vigumu kwake kuendelea na uanachama na kutekeleza majukumu yote mawili.

Mara baada ya barua hiyo, mjadala wa sababu hasa ya kiongozi huyo ambaye alipata kuwa pia mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kabla ya kufukuzwa uanachama ulipamba moto huku wengine wakienda mbali zaidi kwa kusema kuwa hizo ni harakati zake za kujiweka sawa kuwania kiti cha ubunge mwaka 2020 kwa tiketi ya chama tawala cha CCM.

Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya kisiasa walilidokeza gazeti hili sababu nne za kiongozi huyo kuamua kung’atuka uanachama wake kuwa ni pamoja na kutoaminika serikalini.

Mmoja wa watumishi wa wizara hiyo alilimbia Gazeti la Mwananchi kuwa tangu kuteuliwa kwa katibu mkuu huyo wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji amekuwa akikumbana na wakati mgumu serikalini kwani watumishi pamoja na viongozi wenzake hawamuamini na kumuona mtu hatari kufanya naye kazi.

“Hali hii ina mkwaza kikazi, wakati viongozi wenzake wakifanya maamuzi ya pamoja yeye wanamtenga, amekua kama yatima. hana uwezo wa kupata taarifa hata wanapokutana kwani wanamuona si mmoja wao,” kilisema chanzo cha habari.

Sababu nyingine ni kutoonekana timu Magufuli na kushindwa kupata fursa ya kuwa karibu naye kwa kuwa hawaoni kama ni mmoja wao licha ya kuwa katika Serikali.

Walisema kutoka kwake upinzani kulimnyima fursa kubwa ya kuwa karibu na Rais hivyo kujikuta akishindwa kupata fursa hiyo na kujikuta mpweke.

Inaelezwa pia kuwa hali hiyo imesababisha kiongozi huyo katika kipindi cha miezi sita alichokaa katika wizara hiyo kujikuta akiwa muathirika kwa kukosa nyaraka mbalimbali muhimu kutokana kutoaminika kwake na kujikuta yatima.

Sababu nyingine inayotajwa ni hatua ya Zitto Kabwe kuchukua nafasi kukosoa utawala kama alivyokuwa akifanya Mbunge wa Singida Mjini, Tundu Lissu ambaye hivi karibuni alijeruhiwa kwa risasi na watu wasiofahamika.

Inaelezwa hatua ya Zitto kuhoji na kukosoa utawala wa Serikali pamoja na Bunge katika mitandao ya kijamii na katika hotuba zake imesababisha katibu mkuu huyo kuonekana wazi kuwa ameshindwa kumdhibiti kiongozi huyo mkuu wa ACT- Wazalendo.

Inasemekana kwamba hatua hiyo ya Zitto imemuweka katika wakati mgumu Profesa Kitila ambaye ameonekana wazi hawezi kuisaidia Serikali na kwamba hata baada ya kujaribu mara kwa mara kumnyamazisha ilishindika hivyo akaona ni vyema kukaa pembeni ili asinoekane ni mmoja wao.

Sababu nyingine inayotajwa ni uamuzi wake wa kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Ubungo kwa tiketi ya chama tawala.

Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo ameamua kuwekeza nduvu zake kugombea nafasi hiyo ya ubunge ili kupambana na mbunge aliyekuwepo Saed Kubenea.

Mwenyewe afunguka

Mwananchi ilipomtafuta kujibu taarifa hizo, Profesa Kitila alisema hawezi kuzuia watu kuzungumza ila ukweli utabaki pale pale.

“Watu wana mengi yakuzungumza, wana haki ya kufanya hivyo lakini ukweli sababu ziko wazi nimeziweka katika barua yangu ya kung’atuka waisome wataielewa,”alisisitiza Profesa Kitila.

Profesa Kitila alisema kwa upande wake hakufikia uamuzi huo peke yake na kwamba aliwashirikisha viongozi wenzake na wote kwa pamoja walikubaliana.

“Tulikaa na viongozi wenzangu, tukajadili na kuwaeleza sababu za mimi kufikia uamuzi huu nao bila hiyana walikubaliana na mimi na wakabariki kitendo hiko ndipo nilipoandika barua. Kwahiyo ninachotaka watu wajue tu siyo uamuzi wangu mwenyewe.”

Alisema kilicho msukuma zaidi baada ya kupata ugumu pale anapotekeleza na kusimamia mipango na mafanikio ya Serikali ambayo yeye ni sehemu yake hivyo ili kuepuka mgongano wa wazi wa masilahi (confilict of interest), ameamua kung’atuka uanachama wake.

Hata hivyo, kiongozi mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe alipoulizwa na gazeti hili hakuwa tayari kulizungumzia hilo.

Awali ofisa habari wa chama hicho, Abdallah Khamis alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia suala hilo alisema kujiondoa kwa mtu kwenye chama au kubaki ni utashi wake.

Profesa Kitila Mkumbo ni nani?

Alizaliwa 21 Juni 1971 katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba mkoani Singida.

Elimu

Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko Wilaya ya Iramba kati ya mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya Sekondari Mwenge (Singida) na kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1988-1991 na elimu ya Juu ya Sekondari akaipata pale Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka 1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).

Baada ya kuhitimu kidato cha sita alifanya kazi ya kuvua samaki katika Bwawa la Mtera huko Iringa kwa sababu ya kuwa na hali mbaya ya kiuchumi na baadaye alipata nafasi ya kwenda kujiunga na mafunzo ya polisi kwenye Chuo cha Polisi(CCP) Moshi kwa muda wa miezi miwili lakini alikatisha mafunzo baada ya kuchaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM)

Alihitimu shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1999 akisomea Sayansi ya Elimu.

Baada ya kumaliza alianza kazi hapo hapo chuo kikuu kama Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 – 2003) na wakati anafanya kazi aliendelea kusoma Shahada ya Uzamili (M.A) akibobea katika Saikolojia, alihitimu shahada hiyo mwaka 2002.

Profesa Kitila alifanya vizuri katika shahada ya uzamili na baada ya kufundisha chuo kikuu kwa miaka michache alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha Southampton kilichoko nchini Uingereza ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamivu akibobea pia katika saikolojia, hii ilikuwa ni mwaka 2008.

Kati ya mwaka 2009 – 2012, Profesa Kitila amefanya kazi kama mratibu wa kamati ndogo ya ufundi ya masuala ya ukimwi Mwaka 2010 hadi 2012 amekuwa Makamu Mwenyekiti wa UDASA (Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na kisha akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake.

Mwaka 2009 alikuwa Ofisa anayesimamia mitihani katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia, amekuwa mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na masomo ya Mtaala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 2009 – 2012, amekuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE) na kuwa Profesa Mshiriki katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuanzia Julai 2014.

Siasa

Profesa Kitila alianza siasa kama mwanachama wa CCM, baadaye alijiunga Chadema kawa mshauri muhimu wa chama hicho.

Mwaka 2014, Profesa Kitila alifukuzwa katika chama chake cha Chadema kwa tuhuma za kuandaa waraka wa mapinduzi na kukihujumu chama hicho, Kitila alitangaza kuwa angeshirikiana na Zitto Kabwe kuanzisha chama kipya ambacho hivi sasa kinajukana kama ACT – Wazalendo.

Mwaka 2017 Rais John Magufuli alimteua Profesa Kitila kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji nafasi ambayo anahudumu mpaka sasa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad