Takukuru Yatekeleza Amri ya Mahakama Yampeleka Sethi Muhimbili

Taakukuru Yatekeleza Amri ya Mhakama Yampeleka Sethi Muhimbili
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imetekeleza amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kumpeleka mshtakiwa wa kesi ya uhujumu uchumi, Harbinder Sethi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kufanyiwa vipimo.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai jana alimweleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokwenda kutajwa.

Alieleza kuwa wametekeleza amri za mahakama walizopewa kwa kumpeleka Sethi Muhimbili na kwamba kinachosubiriwa ni ripoti ya daktari.

Naye wakili wa mshtakiwa James Rugemalira, Respicius Didas alieleza kuwa kuna ucheleweshaji wa upelelezi na kwamba washtakiwa walifikishwa mahakamani tangu Juni 19 na wapo ndani hadi sasa.

Wakili Didas alidai kuwa kila kesi ikifika mahakamani upande wa mashtaka unawaambia upelelezi bado, wateja wao wanaendelea kukaa ndani na wameathirika. Akijibu hoja hiyo, Swai alidai uchunguzi wa kesi ya kughushi unachukua muda na sheria ipo wazi.

Sethi na Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka matano ya kutakatisha fedha pamoja na kusababisha hasara ya Dola 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 27 kesi hiyo itakapotajwa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad