Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Morogoro, Beutoz Mbwiga amewataka wanaolalamika kuhusu rushwa katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa ushirikiano ili wahusika wakamatwe.
Tangu kuanza uchaguzi takriban miezi mitatu iliyopita Takukuru mkoani Morogoro imewahoji wanachama zaidi ya 10 wa CCM kutokana na malalamiko ya kutoa au kupokea rushwa lakini haijamfikisha yeyote mahakamani kutokana na tuhuma hizo kushindwa kuthibitishwa.
Kamanda Mbwiga akizungumza na Mwananchi amesema taasisi hiyo imekuwa ikipokea malalamiko kwa njia ya simu na maandishi kuhusu uwepo wa rushwa katika uchaguzi lakini wanapofuatilia wanashindwa kuthibitisha.
“Niwaombe wana CCM wanaolalamika watupe ushirikiano ili tuwatie hatiani wahusika, wanatupigia simu na tunatuma watu wetu kwa siri kwenye uchaguzi lakini hakuna ushahidi kama kuna rushwa inatolewa,” amesema Mbwiga.
Amesema kupambana na rushwa kunahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi wanaolalamika.
Kamanda Mbwiga amezitaja wilaya zinazoongoza kwa malalamiko ya rushwa kuwa ni Kilombero, Morogoro Mjini, Morogoro Vijijini, Gairo na Mvomero.
Amesema Takukuru pia imekuwa ikikabiliwa na changamoto inapomwita mwanachama au mgombea kumhoji wamekuwa wakilalamika kuwa inatumika kuwadhoofisha katika uchaguzi.
Akizungumzia rushwa katika uchaguzi, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya katibu wa uenezi wilaya ya Mvomero, Abdallah Bozo amesema vitendo hivyo vilijitokeza na hakuna hatua zilizochukuliwa.
Mwanachama wa CCM, Rashid Abdallah mkazi wa Mvomero ameilaumu Takukuru kwa kutochukua hatua.
Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Kulwa Milonge amesema chama hicho kimesimama katika nafasi yake kuhakikisha hakuna kiongozi anayepatikana kwa kutoa rushwa.
Amesema kanuni za maadili za CCM ziko wazi kuwa ikibainika mgombea alitumia rushwa kupata ushindi ataondolewa na uchaguzi utarudiwa.