Tanroad Yabomoa Nyumba ya Prof. Jay

Tanroad Wabomoa Nyumba ya Prof. Jay
NYUMBA ya Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu kama Prof. Jay, katika eneo la Mbezi Kimara imebomolewa na Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), kwa kile kilichoelezwa imejengwa kwenye hifadhi ya barabara ya Chalinze Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ni maandishi kwenye akaunti ya Instagramu ya mbunge huyo, nyumba hiyo ilibomolewa bila yeye kupewa taarifa.

Nipashe ilimtafuta Profesa Jay kwa simu zake, lakini hazikupatikana na hata kwa WhatsApp iliita bila kupokelewa na alivyotumiwa ujumbe wa maandishi haukujibiwa.

Taarifa za kubomolewa alizipokea kutoka kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), waliompigia baada ya saa 24 nyumba kubomolewa wakimtaarifu wanakwenda kukata umeme na kuchukua mita yao.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Magomeni, Frank Chambua, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, alithibitisha nyumba ya Mbunge huyo kubomolewa Ijumaa na Tanesco walikwenda kuchukua mita na nyaya zao zilizokuwapo na kuzirejesha ofisini.

“Jana (juzi) tulikwenda kwenye eneo na kukuta nyumba yote imeshabomolewa, tulichukua mita na nyaya zetu na kuzirejesha ofisini, nasi tulijulishwa baada ya nyumba kubomolewa,” alieleza.

Meneja huyo alisema kwa mujibu wa utaratibu Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wanapokwenda kubomoa nyumba huwajulisha, ili wakate umeme, nao huwajulisha wateja, ili waruhusiwe kuingia kuchukua mita na nyaya.

“Kuna maeneo mengine mazingira yanakuwa magumu sana kwamba ni lazima kuwajulisha wateja wetu watusaidie tuchukue nyaya na mita, maana nyingine zinabomolewa nusu na nusu inabaki na nyingine zinakuwa ndani ya ukuta, huwezi kuingia bila ruhusa ya mwenye nyumba,” alifafanua Meneja huyo.

Katika ujumbe wake Prof. Jay ambaye pia ni Msanii wa Bongo Flavor, alisema: “Mimi ni mmoja wa waathirika wa hili zoezi la kubomolewa nyumba zetu huku Mbezi Kimara Septemba 29, mwaka huu.”

Aliongeza: “Jana (siku alipoandika ujumbe) nikiwa katika majukumu jimboni Mikumi majira ya saa 12 jioni, nilitaarifiwa kwamba watu wa Tanroads wakiwa wameambatana na greda mbili na magari mawili ya polisi (defender) yenye askari waliokuwa na silaha mbalimbali za moto walikuwa wanabomoa nyumba yangu (sijawahi kuumia kiasi hiki).”

“Nimesikitishwa sana jinsi Tanroads wanavyoweza kujichukulia maamuzi bila kujali mhimili muhimu wa mahakama, wametoa maagizo gani. Na taratibu zilizotumiwa kubomoa nyumba yangu bila ya mimi na Tanesco kupewa taarifa na kubomoa huku umeme unawaka kilikuwa ni kitendo kinachohatarisha maisha ya wabomoaji wenyewe, familia yangu na majirani zangu.”

Haule alisema Tanesco walimpigia saa 24 au zaidi baada ya ubomoaji wakimtaarifu wanakwenda kukata umeme kabla ya ubomoaji, lakini aliwajulisha kuwa imeshabomolewa.

“Niliwaambia imeshabomolewa kabisa, sijaweza kuokoa kitu chochote hata mita yenu mnayoiulizia mkaitafute kwenye kile kifusi cha nyumba yangu kilichokusanywa na Tanroads. Tanesco walishangazwa sana kuvunjwa nyumba yangu kwa taratibu hizo,” alisema.

“Lakini naamini kila kitu kinatokea kwa sababu maalum. Nimejifunza kumtegemea Mungu na kumshukuru kwa kila jambo, na hili moja ya mitihani ya hapa duniani, nimepokea na kumsikiliza Mungu ana mpango gani juu yetu katika familia yangu mbeleni. Tumelipokea na naamini tutashinda,” alisema zaidi.

Meneja huyo alisema: “Tanroads walitupa taarifa tukatoe mita za umeme, na mara nyingi wanaweza kupiga na tukifika eneo la tukio tunakuta wanaendelea kubomoa nyumba,” alisema na kuendelea:

“Kama nyumba itavunjwa nusu na nusu kubaki tunamrejeshea mita mteja baada ya kujiridhisha kutoka Tanroads, ila kama inavunjwa yote huwa tunawahi kuchukua mita na nyaya zetu na haiamishwi kwenda eneo jingine hata akijenga nyumba kwingine.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad