Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu jana alikuwa jijini Nairobi nchini Kenya ambapo alikwenda kuchukua dawa kwa ajili ya mgonjwa Samson Mwanga ambaye alipasuka mshipa wa kichwa ametangaza kuwa mgonjwa huyo amepoteza maisha alfajiri ya leo.
Nyarandu amesema kuwa mgonjwa huyo Samson Mwanga amefariki dunia alfajiri ya leo akiwa katika Hospitali ya rufaa ya KCMC iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro
"Nilikuwa hospitali ya KCMC, Moshi saa 7:00 usiku kuamkia leo kupeleka dawa (Intravenous Immunoglobulin) nilizozitoa Nairobi Hospital na kuzisafirisha usiku kwa ajili ya kuendelea kumtibu mgonjwa Samson Mwanga tuliyemrusha kwa ndege toka Hydom Hospital Jumanne iliyopita. Kwa bahati mbaya sana, tumempoteza Samson alfajiri majira ya 11:00 asubuhi" alisema Nyalandu
Aidha Mbunge huyo wa Singida Kaskazini ametoa shukrani zake kwa madaktari wa KCMC kwa kila walichoweza kufanya ili kuweza kuokoa maisha ya Samson mbaka pale umauti ulipomkuta alfajiri ya leo.
Septemba 26, 2017 Lazaro Nyalandu aliweza kufanikisha safari ya Samson kutoka katika hospitali ya Hyadom na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Kilimanjaro kwa dharura kutokana na mgonjwa huyo kupasuka mshipa wa kichwa hivyo alipelekwa KCMC kwa matibabu zaidi lakini leo amepoteza maisha akiwa bado anapatiwa matibabu.
Bwana ametoa, na Bwana ametwaa, jina la bwana lihimidiwe