TPSF: Serikali Inapaswa Kuufanyia Kazi Ushauri wa Dngotena Si Kuupuuza

TPSF: Serikali Inapaswa Kuufanyia Kazi Ushauri wa Dngotena Si Kuupuuza
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imesema Serikali inapaswa kuufanyia kazi na si kuupuuza ushauri uliotolewa na bilionea namba moja barani Afrika, Aliko Dangote.

Juzi, Dangote alimtahadharisha Rais John Magufuli kuwa vitendo vyake vinaogofya na kukimbiza wawekezaji nchini.

Dangote alilaumu sera za Serikali akisema, “zinawatisha wawekezaji wengi. Kuwatisha wawekezaji si kitu kizuri. Mmoja akitishwa wengine watakimbia bila hata kuhitaji maelezo.”

Malalamiko hayo aliyatoa jijini London, Uingereza anakohudhuria kongamano la wawekezaji wa Afrika lililoandaliwa na gazeti la Financial Times.

Akitoa maoni yake jana kuhusu kauli hiyo ya Dangote, mkurugenzi mkuu wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema mwekezaji huyo ni mkubwa na anapozungumza anasikika ndani na nje ya Afrika hivyo kutoufanyia kazi ushauri wake kunaweza kuligharimu Taifa.

“Alichokisema ni ushauri tu, Dangote ni mwekezaji mkubwa, amewekeza ndani na nje ya Afrika. Sidhani kama ushauri wake unaweza usifanyiwe kazi na mimi nashauri ufanyiwe kazi si kuupuuza,” alisema Simbeye na kuongeza:

“Serikali iufanyie kazi kama ana hoja zifanyiwe kazi si kuzipuuza na kama hana hoja ajibiwe, yule si mtu wa kumbeza. Mtu kama huyu mwekezaji mkubwa anapozungumza kitu tunapaswa kukiona na kukifanyia kazi, ni wakati wa Serikali kuupokea ushauri wake.”

Simbeye alisema kwa uzoefu wake katika nchi mbalimbali anachokizungumza mfanyabiashara huyo kina tija hivyo ni wakati sasa Serikali kupokea ushauri huo.

Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto alisema Serikali isikilize na kufanyia kazi mawazo ya sekta binafsi katika kuweka sawa mazingira ya uwekezaji bila kupoka haki ya nchi kufaidika na rasilimali zake.

“Kwa mfano hoja aliyotoa ndugu Dangote si ya kupuuza kwani kwa kawaida mitaji huona aibu. Serikali ijiondoe kwenye mentality (dhana) kuwa uwekezaji ni kupata kodi tu, la hasha,” alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini na kuongeza:

“Kwa demografia ya Tanzania, ambapo watu milioni 1.6 huingia kwenye soko la ajira kwa mwaka, ajira yapaswa kuwa lengo kubwa la Serikali katika kuvutia mitaji kutoka nje na vilevile ndani.”

Zitto pia aliitaka Serikali ifanyie kazi uchumi wa vijijini kwa kurekebisha upungufu wote unaoshusha uzalishaji kwenye sekta ya kilimo ikianza na pembejeo, masoko na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mazao.

Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi alisema ufike wakati wawekezaji wasigeuke miungu watu wadogo huku akiishauri Serikali kuendelea na mikakati yake ya kuimarisha uwekezaji.

“Tumpuuze tu, mazingira ya sasa ya biashara yanahitaji uwazi na ili uwe wazi lazima upinge rushwa na dhana ya ‘win win situation’. Unapomuona mwekezaji kaja kwako kuna kitu kakiona sasa ukiona anaanza kusema vikwazo kuna jambo,” alisema Profesa Moshi.

Alisisitiza kuwa, “sisi tuendelee na tunayoyafanya, wao wanatafuta faida na sisi tunatafuta, ndiyo dhana ileile niliyoisema win win situation. Inawezekana huko nyuma kulikuwa na njia za namna namna ambazo sasa hazipo.”

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema: “Mimi sina ubishi na Dangote na hatuwezi kupuuza ushauri wake kwani uwapo wake nchini umefanikisha kubadili hata bei ya saruji.”

“Nimezungumza na Dangote na amekwisha kuzungumza pia na viongozi wangu wa juu na tunatambua uwekezaji wake hapa nchini,” alisisitiza Mwijage.

Waziri huyo alisema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kusubiri kuhitimishwa kwa majadiliano ya sakata la mchango wa madini (makinikia) kati ya Serikali na wawekezaji wa kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo yatafungua mlango mpya wa sekta hiyo. Dangote amewekeza nchini Dola 500 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.1 trilioni) na anaona sheria hiyo haitendi haki na itawakimbiza wawekezaji.

Malalamiko ya Dangote yanatokana na sheria mpya ya usimamizi wa rasilimali za Taifa iliyopitishwa na Bunge mwezi Julai inayopendekeza Serikali kuwa na walau asilimia 16 kwenye miradi yote iliyowekezwa kwenye sekta ya madini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad