Rais wa Marekani Donald Trump anapanga kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa nyuklia kati ya nchi za Magharibi na Iran, taarifa kwenye vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti.
Iwapo atakataa kuidhinisha mkataba huo, bunge la Congress litalazimika kuamua iwapo litaiwekea tena Iran vikwazo.
Bw Trump ana hadi tarehe 15 Oktoba kufanya uamuzi wake.
Kiongozi huyo alikuwa ameukosoa sana mkataba huo kwenye kampeni za uchaguzi wa urais mwaka jana.
Alipokuwa anapigwa picha akiwa na viongozi wa kijeshi Alhamisi, Trump alisema kuna "utulivu kabla ya tufani" lakini akakosa kutoa maelezo zaidi.
Kulikuwa na fununu kwamba huenda alikuwa anazungumzia kuongezeka kwa uhasama kati ya nchi hiyo na Korea Kaskazini.
Lakini gazeti la New York Times limesema "watu ambao wamepashwa habari kuhusu suala hilo" wanaamini alikuwa anaizungumzia Iran.
Trump alionekana akiwa White House na mke wake, pamoja na viongozi wa jeshi, baada ya mikutano Alhamisi lakini kabla ya chakula cha jioni.
Huku akiashiria kwa vidole watu ambao walimzunguka, aliwauliza wanahabari iwapo wanafahamu "hili linawakilisha nini".
"Pengine ni utulivu kabla ya tufani," alisema.
Wanawahabari walipomsisitizia afafanue ni tufani gani alilokuwa akizungumzia, aliwaambia tu: "Mtagundua."
Trump na Rais wa Iran Hassan Rouhani walishutumiana mkutano wa UN mwezi jana
Alikuwa awali amewaambia maafisa wake wakuu wa ulinzi kwamba anatarajia wampe "njia nyingi mbadala za kijeshi ... kwa haraka zaidi" siku zijazo.
Urusi imesema mkataba huo wa silaha na Iran unafaa kudumishwa jinsi ulivyo.
Waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov alisema taifa lake linatumai kwamba Marekani itafanya uamuzi wa busara bila kuumia upande wowote.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya pia wamesema wanaunga mkono mkataba huo.
Nini kitafanyika sasa?
Vyombo vya habari Marekani vinasema rais huyo Alhamisi ijayo atatangaza kwamba hataidhinisha mkataba huo kwa sababu haujali maslahi ya Marekani kiusalama.
Lakini baadhi ya washauri wake wakuu wa usalama, akiwemo Waziri wa Ulinzi James Mattis wanaonekana kuunga mkono mkataba huo.
Rais wa Marekani hutakiwa kuidhinisha mkataba huo kila baada ya siku 90; na Trump ameuidhinisha mara mbili.
Iwapo atakataa kuuidhinisha wakati huo, bunge la Marekani litakwua na siku 60 kuamua iwapo litaiwekea tena vikwazo Iran.
Vyombo vya habari Marekani vinadokeza kwamba huenda Bunge likaamua kudumisha hali ya sasa bila kuweka vikwazo vipya.
Akiongea kwenye mkutano na wakuu wa jeshi White House, Trump alisema: "Utawala wa Iran huunga mkono ugaidi na umekuwa 'ukiuza nje' ghasia na vurugu kote Mashariki ya Kati."
"Ndio maana ni lazima tufikishe kikomo uchokozi huu wa Iran na ndoto zake za nyuklia. Mtasikia kutoka kwangu karibuni kuhusu Iran."
Mkataba huo wa mwaka 2015 ulitiwa saini kuzuia Iran kustawisha silaha za nyuklia.
Rais wa Marekani hutakiwa na kutoa idhini kwa Bunge la Congress kuendelea kuudumisha kila baada ya siku 90.
Ufaransa, Ujerumani, Uchina, urusi na Uingereza ni wahusika katika mkataba huo ambao uliondoa baadhi ya vikwazo ambavyo viliizuia Iran kufanya biashara masoko ya kimataifa na kuuza mafuta.
Kuondolewa kwa vikwazo hiyo kulitegemea Iran kusitisha mpango wake wa nyuklia.
Inafaa kupunguza shehena yake ya madini ya uranium, na isijenge vinu vingine vya nyuklia kwa miaka 15 na pia iruhusu wakaguzi nchini humo.
Trump amekwua akisema mara nyingi kwa Iran imekiuka "moyo" wa mkataba huo.
Katika hotuba kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Trump aliutaja mkataba huo uliofanikishwa na mtangulzii wake Barack Obama kuwa "aibu kwa Marekani".