Tuapambana Nao kwa Umakini- Omog

Tuapambana Nao kwa Makini- Omog
KUELEKEA mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Jumamosi, Kocha Mkuu wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, amesema “tutapambana nao kwa umakini”.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog, alisema kazi yake sasa ni kurekebisha makosa machache aliyoyaona katika mechi zilizopita, lakini amewaambia wachezaji wake wajiandae kukutana na ushindani kwa sababu Mtibwa Sugar wameonyesha kiwango kizuri kwenye michezo yao yote iliyotangulia.

Omog ambaye klabu yake inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, alisema Mtibwa Sugar ni moja ya timu zinazofanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya kikosi chake "kubomolewa" na klabu mbalimbali zinazoshiriki ligi hiyo kila msimu unapomalizika.

"Tunajiandaa kwenda katika mazoezi ya jioni (jana jioni), soka ni mchezo ambao kila siku unatakiwa kujifunza, ila kikubwa tunawafahamu Mtibwa Sugar, ni moja kati ya timu ngumu na bora Tanzania, tunaiheshimu na tutaingia kuwakabili huku tukifahamu tuko kwenye hadhi inayofanana," alisema Omog.

Kocha huyo alisema pia anataka kushinda mechi hiyo na ile dhidi ya Njombe Mji itakayopigwa Oktoba 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru ili kujiweka kwenye nafasi "huru" ya kujiandaa kuikabili Yanga wakiwa na ari na kasi iliyoimarika.

Naye Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, ametamba kuwa tangu arithi mikoba ya Salum Mayanga, ambaye aliteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa (Taifa Stars) katikati ya msimu uliopita, hajawahi kupoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu dhidi ya timu za Dar es Salaam.

Katwila alisema kuwa mechi hiyo itakuwa na ‘tensheni’ kwa sababu atakayeshinda atafanikiwa kuongoza katika msimamo wa ligi kwa kuwa timu zote zina pointi 11, lakini Simba ikiwa juu kutokana na kuwa na mabao mengi ya kufunga.

" Mechi yetu itakuwa na ushindani mkubwa wa kila mmoja kutaka kumshusha mwenzake katika mbio za kuongoza ligi, nashukuru tangu nipewe timu sijawahi kufungwa na Simba au Yanga, ninajivunia rekodi yangu na ninataka kuilinda," aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa timu hiyo.

Simba na Mtibwa Sugar zitashuka dimbani kila moja ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi tatu na kutoka sare mara mbili katika mechi zao tano walizocheza msimu huu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad