Wananchi wa Kenya wameanza kujitokeza vituoni kwa ajili ya kupigia kura katika uchaguzi wa marudio, huku askari wakilazimika kuondoa vizuizi vilivyowekwa na watu wanaopinga uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo.
Hali ya utulivu imetawala katika maeneo mengi licha ya wasiwasi uliojitokeza awali. Katika baadhi ya miji kulikuwa na idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura tofauti na ilivyokuwa wakati wa uchaguzi wa awali uliofanyika Agosti 8.
Pia kuna watu walioweka vizuizi vya matofali na mawe katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, hasa katika maeneo ya Mtaa wa Kibera jijini Nairobi ambayo ni ngome ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.
Kiongozi huyo jana aliwataka wafuasi wake kubaki nyumbani na kutoshiriki uchaguzi huo.
Barabara inayoelekea kituo cha Shule ya Msingi ya Olympic ilifungwa na polisi walilazimika kutumia nguvu za ziada kuondoa mawe na matofali yaliyokuwa yamepangwa barabarani.
Katika maeneo ya miji ya Kusumu na Mombasa ambayo ni ngome kuu ya Odinga, kumekuwa na idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupiga kura huku maofisa wa Tume ya Uchaguzi wakiwa wanasubiria wapigakura.
Rais Uhuru Kenyatta amesema hali ya usalama itaimarishwa nchini kote na amewataka Wakenya kwenda kupiga kura, huku wakizingatia haki za wale ambao hawataki kushiriki kupiga kura