Uchaguzi wa Rais Kuendelea Kenya Kurudiwa Vituo Vitano Leo

Uchaguzi wa Rais Kuendelea Kenya Kurudiwa Vituo Vitano Leo
Uchaguzi wa marudio ambao ulipangiwa kufanyika leo nchini Kenya katika maeneo ambayo shughuli hiyo haikufanyika Alhamisi utafanyika katika vituo vya kupigia kura vitano pekee.
Vituo hivyo ambavyo vina jumla ya wapiga kura 696 vinapatikana katika eneo bunge la Turkana ya Kati, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC Wafula Chebukati alisema tume hiyo haingeweza kuendelea na uchaguzi katika vituo vingine 3,635 ambavyo vinapatikana katika maeneo bunge 27, mengi yakiwa ngome ya muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa).
Kiongozi wa muungano huo, waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, alisusia uchaguzi huo na alikuwa amewataka wafuasi wake kutoshiriki.
Mengi ya maeneo bunge hayo yanapatikana katika majimbo manne - Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya.
Bw Chebukati alisema tarehe ambayo uchaguzi utafanyika maeneo hayo itatangazwa baadaye ingawa hakusema ni lini.

"Jana, baadhi ya wafanyakazi wangu walitekwa na kuteswa. Baadhi nyumba zao zilivunjwa na kuporwa. Wengine waliamrishwa kutofika na kuzuiwa kwa nguvu kufika vituo vya kupigia kura ambapo walifukuzwa. Baadhi wametafuta hifadhi katika vituo vya polisi," alisema Bw Chebukati katika taarifa Ijumaa jioni.
"Katika baadhi ya visa, hata polisi zaidi waliotumwa kuimarisha usalama hawakuweza kuzuia ghasia kwani fujo kutoka kwa waandamanaji pia zilizidi."
Wasifu wa Raila Odinga, kiongozi wa upinzani Kenya
Mfahamu rais 'wa kidijitali' Uhuru Kenyatta
Mwenyekiti huyo wa tume aliwalaumu wanasiasa na kutoa wito kwao kuhakikisha "watu kutoka maeneo yaliyoathiriwa hawanyimwi haki yao ya kupiga kura na pia kuhakikisha haki ya kuishi inaheshimiwa."
"Uchaguzi wa kufana ni matokeo ya watu mbalimbali wakifanya majukumu yao na bila ubinafsi na kwa njia njema. Hii ni pamoja na viongozi wa kisiasa, maafisa wa usalama na wanahabari."
Siaya Migori
Tume ya IEBC ilikuwa awali imekadiria kwamba asilimia 48 ya wapiga kura 19.6m waliosajiliwa kupiga kura walishiriki uchaguzi huo.
Hii iliashiria kuwa huenda hadi watu 9.4m walijitokeza kushiriki, idadi ambayo ni ya chini mno ukilinganisha na uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ambapo waliojitokeza walikuwa asilimia 78.9 ambao ni wapiga kura 15m.
Lakini Bw Chebukati baadaye alifafanua kwamba takwimu halisi kutoka maeneo bunge 267 zilikuwa zinaonesha waliokuwa wamejitokeza maeneo hayo walikuwa 6.6m.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad