Ufafanuzi wa Polisi Kuhusu Utoaji wa Stika za Usalama Barabarani


Kikosi cha Usalama Barabarani, kimekanusha taarifa inayosambazwa mitandaoni kuhusu ugawaji wa stika za usalama barabarani na kusema hazina ukweli wowote badala yake zipuuzwe.

Hayo yamesemwa na kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu na kueleza kuwa ukaguzi wa vyombo vyote vya usafiri na usafirishaji umeanza leo Jumanne Oktoba 17, 2017, baada ya uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama uliofanywa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, jana Jumatatu, katika mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Musilimu amesema kuwa taarifa hizo siyo za kweli na ukaguzi wa magari ni wa lazima na utafanyika nchi nzima.

Taarifa hiyo iliyosambazwa inaeleza kuwa ukaguzi wa magari madogo utalipiwa Sh. 15,000 huku magari makubwa yakilipiwa Sh. 30,000 na stika itauzwa kwa Sh. 8,000.

Musilimu amesema kuwa ukaguzi huo utafanyika kwa awamu kwa kuhusisha magari ya abiria na ya mizigo na utafanyikia katika sehemu husika kama vile, vituo vya mabasi, gereji, vituo vya polisi na maeneo mengine yatakayotangazwa na Mkoa husika.

“Magari ya mizigo na ya abiria ndiyo yataanza kwa muda wa miezi mitatu ya ukaguzi na ubandikaji wa stika. Hapa tunajumuisha daladala, mabasi ya abiria, malori na teksi. Magari mengine madogo yatatangaziwa muda maalumu,” alisema Kamanda.

Kamanda Musilimu amesema kwamba magari yote yanayotembea barabarani ni lazima yawe salama na stika itatolewa tu baada ya Afisa atakayelikagua kuridhishwa na hali ya usalama wake na mhusika atatakiwa kulipo Sh. 5,000 tu.

“Maofisa wetu watakuwepo sehemu maalumu iliyopangwa. Kifungu cha 39 cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 inasema gari linalotembea ni lazima liwe salama, hivyo stika zote zitatolewa baada ya ukaguzi na kupewa fomu ya polisi namba 93 inayoonyesha chombo chako ni salama,” alisema Kamanda Musilimu.

Kuhusiana na taasisi pamoja na Kampuni binafsi, Kamanda Musilimi amesema zinaweza kuomba kupatiwa huduma ya ukaguzi katika maeneo yao na kwamba baada ya zoezi la ukaguzi kuisha operesheni kubwa itafanyika kubaini magari ambayo hayakukaguliwa kisha kuyakamata.

“Mashirika makubwa wanayo nafasi ya kuomba kukaguliwa mahali walipo nasi tutawafuata. Kipindi hicho kikipita operesheni kubwa ya kukamata vyombo hivyo itafuata,” alisema Kamanda Fortunatus.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad