Ujangili wa kutumia waya katika hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Hifadhi za Jamii (WMA), umechangia kupungua kwa wanyama wakiwamo nyumbu kwa asilimia 40 katika ikolojia ya Serengeti.
Nyumbu ni kati ya vivutio vinavyoifanya Hifadhi ya Serengeti kuwa kwenye maajabu ya dunia kutokana na jinsi wanavyohama kwa kuvuka Mto Mara kwenda Maasai Mara nchini Kenya na kurudi.
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) cha Hifadhi ya Serengeti, Dk Robert Fyumagwa alisema juzi kuwa hali si nzuri.
Dk Fyumagwa alitoa kauli hiyo katika mdahalo wa wadau wa hifadhi ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, chini ya uratibu wa Frankfurt Zological Society, Serengeti Media Centre na Chuo cha Utalii (Setco).
“Nyumbu wamepungua kutokana na ujangili wa nyaya unaofanywa na jamii inayozunguka ikolojia hiyo ambayo inasema inamuenzi Mwalimu Nyerere, ikumbukwe yeye alikemea ufujaji wa mali za umma na kila mwananchi ana wajibu wa kulinda maliasili zetu,”alisema.
Meneja wa Mradi wa Frankfurt Zological Society, Masegeri Tumbuya alisema kuwa tangu Aprili hadi Septemba mwaka huu, mitego 6,837 ya nyaya iliteguliwa katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia kitengo maalumu kinachoshughulika na udhibiti wa ujangili huo.