Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) umefutilia mbali maandamano ambayo yalikuwa yamepangiwa kufanyika nchini humo leo kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi.
Muungano huo, kupitia taarifa, umesema umechukua hatua hiyo kupata fursa ya kuomboleza watu ambao wameuawa kwenye maandamano ya awali.
Nasa, muungano unaoongozwa na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, ulikuwa umeahidi kufanya maandamano kila siku kushinikiza mageuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.
Taarifa iliyotumwa na msemaji wa Bw Odinga, Dennis Onyango, imesema maandamano hayo yatarejelewa tena Jumatano.
Uchaguzi mkuu umepangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba baada ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti na kuagiza uchaguzi mpya wa urais ufanyike katika kipindi cha siku 60.
"Hii ni hatua ya muda ya kuuwezesha muungano huu kuwazuru na wafuasi wake waliokumbana na ukatili wa polisi na jamaa za waliojeruhiwa au kuuawa," taarifa hiyo ilisema.
Jumatatu, kijana wa miaka 18 aliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani mjini Kisumu.