Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Profesa Joe Lugalla amesema ushirikiano wa kielimu unaoendelea katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umekifanya chuo hicho kunufaika kwenye masuala ya uongozi, ulinzi, dini na elimu.
Profesa Lugalla amesema hayo jana Jumatatu Oktoba 23,2017 katika mkutano wa pili wa mwaka wa kujadili masuala ya taaluma kwa walimu uliofanyika nchini Uganda.
Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Elimu ya Juu wa Uganda, John Muyingo ukiwa na kauli mbiu ya “Kufikiria upya taaluma kwa walimu.”
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 24,2017 na AKU imesema mkutano huo ni wa siku mbili.
Profesa Lugalla amesema AKU na Taasisi ya Kuendeleza Elimu Afrika Mashariki (IED-EA) zimejikita kutoa elimu bora na yenye manufaa kwa jamii. Amesema ushirikiano ni chachu ya kufikia malengo yao.
“Utoaji wa elimu ni sera ya kidunia inayohitaji ushirikishwaji na ushirikiano baina ya mataifa. Tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja si katika kutoa mawazo ya jinsi ya kufikiria upya taaluma kwa walimu bali katika utekelezaji wake,” amesema Profesa Lugalla ambaye pia ni Mkurugenzi wa IED-EA.
Waziri Muyingo amekipongeza Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa uongozi imara katika masuala ya elimu na afya nchini Uganda.
Amesema ni muhimu kuifanya taaluma ya ualimu kuwa ya kipekee.
“Natambua jitihada za Serikali pekee hazitoshi katika kuboresha, kuvumbua na kubadilisha taaluma ya elimu katika nchi yetu. Jitihada za sekta binafsi na wadau wengine bado zinahitajika kwa kiasi kikubwa,” amesema Muyingo.