Uteuzi wa Rais Magufuli Kupingwa Mahakamani


Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa Katibu wa Itikadi, Mawasialiano na Uenezi, Ado Shaibu kimesema kuwa kitakwenda mahakamani kupata ufafanuzi wa kina kuhusu kile walichodai ni kukiukwa kwa sheria katika uteuzi wa Katibu wa Bunge uliofanywa na Rais jana Oktoba 7, 2017.

Katika taarifa iliyotoleo leo na chama hicho, imeeleza kwamba, “Kama Rais hatatengua uteuzi huu na kufuata utaratibu uliowekwa na sheria za nchi, ACT Wazalendo kitalifikisha suala hili mahakamani ili kupata ufafanuzi wa mahakama.”

Wakati akitangaza mabadiliko katika baraza la mawaziri, Rais Magufuli alitangaza pia kumteua Stephen Kigaigai kuwa Katibu wa Bunge, na kwamba katibu aliyekuwepo, Dk. Thomas Kashililah atapangiwa kazi nyingine.

ACT Wazalendo wamesema uteuzi huo ni kinyume na sheria kwa sababu, mbali na Rais kuwa na mamlaka ya kumteua Katibu wa Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 87 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anapaswa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Sheria ya Utawala wa Bunge – The National Assembly (Admintration Act), 2015. Kwa mujibu wa Kifungu cha 7(3) cha Sheria hiyo, Rais atateua jina moja kutoka miongoni mwa majina matatu yaliyopendekezwa na Tume ya Huduma za Bunge.

Kwa mujibu wa ACT wamesema, hakuna kikao chochote cha Tume ya Bunge kilichoketi na kupendekeza majina kwa Rais kwa ajili ya uteuzi wa Katibu wa Bunge. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wote wa Tume ya Huduma za Bunge waliohojiwa na vyombo vya habari wamethibitisha pia kutofanyika kwa kikao hicho.

“ACT Wazalendo tunaona kuwa uteuzi huu si tu ni mwendelezo wa Rais kufanya maamuzi bila kuzingatia sheria za nchi bali ni ushahidi mwingine wa wazi wa kudharau mhimili wa Bunge,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, chama hicho kimemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuishauri serikali kwenye masuala ya kisheria kuwajibika, lakini pia wakamataka mwanasheria mkuu kujiuzulu endapo ushauri wake kwa serikali hauthaminiwi.

“Inawezekana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa woga au uzembe, hamshauri Rais ipasavyo au Rais hafuati ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika yote mawili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kama anataka kulinda heshima yake binafsi na ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hana budi KUJIUZULU.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad