Video ya Lissu Akizungumza Inatarajiwa Kutolewa Leo

Video ya Lissu Akizungumza Inatarajiwa Kutolewa Leo
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alizungumza na waandishi wa habari kueleza kuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameinuka kitandani na ametoka ICU, lakini dokezo kwamba video inayomuonyesha akizungumza itatolewa leo, limeibua shauku ya kipekee na kuwa gumzo.

Taarifa ya video ya Lissu imeibua hamu ya watu kutaka kuiona, huku viongozi wa Chadema wakionekana kutokuwa tayari kuitoa hadi hapo ujumbe uliotolewa jana kuhusu hali yake utakapofika kwa wananchi.

Lissu, ambaye ni mwanasheria mkuu wa Chadema, alishambuliwa kwa risasi zipatazo 32 akiwa ndani ya gari , nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma, ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka kikao cha asubuhi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Hadi sasa, Jashi la Polisi halijatangaza kumshikilia mtu yeyote kwa kumuhusisha na shambulio hilo lililotokea Septemba 7 katika eneo la makazi ya viongozi ambayo yana ulinzi.

Alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na usiku alisafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi, ambako alikuwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) hadi mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Mgonjwa ameimarika na kuanzia leo (jana) tutaanza kutoa picha zake,” alisema Mbowe alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema.

“Kwa mwezi mmoja na nusu hatujawahi kutoa picha ila kuanzia leo (jana) au muda mfupi ujao tegeni masikio mtasikia sauti yake (Lissu) na mtaiona sura yake.”

Tangu aanze kupata fahamu, watu ambao wamekuwa wakienda Nairobi kumjulia hali wamekuwa wakieleza jinsi Lissu anavyowatia moyo na kuwapa ujasiri wa kuendelea kupigania demokrasia.

Baadhi yao wamerejea na kauli za kijasiri, lakini sauti ya mwanasheria huyo wa kujitegemea, wala picha yake haijawahi kuonekana tangu Septemba 7 usiku alipokuwa akipandishwa kwenye ndege kuhamishiwa Nairobi.

Ingawa Mbowe hakutaka kuweka bayana ujumbe aliosema Lissu kwenye video hiyo, Mwananchi imedokezwa na kigogo mmoja wa chama hicho kwamba inamwonyesha akitoa salamu kwa Watanzania na wananchi wa ndani na nje ya nchi.

Alisema Lissu atazungumzia kwa ufupi hali yake na msimamo wake katika harakati ambazo anadai zimemfikisha hapo.

Hali ya Lissu

Katika mkutano huo, Mbowe alisema Lissu ametoka ICU, anakula chakula anachokitaka bila kutumia mirija na anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu.

Alisema Lissu amekamilisha awamu ya pili ya matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji mara 17 kuondoa risasi zilizoingia na kutoka ndani ya mwili wake na siku yoyote kuanzia wiki ijayo atapelekwa nje ya Kenya kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, hakueleza nchi gani ingawa sehemu ambazo wagonjwa wengi wamekuwa wakipelekwa ni Afrika Kusini, Ujerumani, India na kwa nadra Marekani.

“Lissu mpaka sasa amefanyiwa upasuaji mkubwa mara 17, ameongezewa damu nyingi kuliko mgonjwa yeyote aliyewahi kutibiwa Hospitali ya Nairobi kwa miaka 20 iliyopita,” alisema Mbowe

“Wiki iliyopita, Lissu ametoka ICU na juzi kwa mara ya kwanza alikaa. Anatumia ‘wheel chair’ na aliliona jua kwa mara ya kwanza,” alisema huku wanachama waliohudhuria mkutano huo wakionekana kufurahi na wengine kushtuka.

Mbowe, huku akizungumza kwa sauti ya chini na yenye hisia, alisema: “Lissu hatumii tena hewa ya oxygen wala mirija na anakula chakula anachokitaka mwenyewe. Tunawashukuru madaktari wa Dodoma na wa Nairobi kwa kuakoa maisha yake.”

Mwenyekiti huyo alisema baada ya chama hicho kushiriki kwa ukaribu zaidi katika awamu ya kwanza na ya pili, jukumu la usimamizi wa matibabu ya awamu ya tatu yatakayofanyika nje ya Nairobi wataiachia familia ila wao watakuwa nyuma ya familia.

“Tunaishukuru sana familia ya Lissu imekuwa na msimamo kama Lissu mwenyewe. Tumefanya kazi na familia na tutaendelea kufanya kazi na familia,” alisema Mbowe.

“Tutakapokwenda katika matibabu ya tatu, tutaiacha kwa familia iwe msemaji wa kwanza. Mgonjwa anaweza kuongea na anajitambua.”

Alisema suala la gharama kulipiwa na Serikali si hisani kwani Lissu ni mbunge na anastahili, lakini akasema si kwa masimango na kwamba tayari Lissu na familia walishalizungumzia hilo.

Uchunguzi wa nje

Kuhusu uchunguzi wa tukio hilo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliendelea na msimamo kwamba ili kupata ukweli wa tukio hilo na mengine, lazima ufanywe na  vyombo vya nje.

“Lissu aliposhambuliwa ilichukua masaa mawili polisi kufika eneo la tukio. Kwa nini tusiingie hofu kuwa ulikuwa ni mkakati wa makusudi wa kuwatoa wale waliohusika,” alisema Mbowe.

“Bado tunasisitiza uchunguzi ufanywe na vyombo huru vya nje. Hatuna imani na vyombo vya ndani.

Unajiuliza, Mheshimiwa Lissu ni jirani wa waziri, tuna taarifa kuwa ile CCTV  Camera iliyokuwepo eneo la tukio imeondolewa, imeondolewa na nani?”

Alisema jeshi la polisi halipaswi kutoa visingizio kwamba limeshindwa kuendelea na uchunguzi kwa sababu dereva wa Lissu yupo Nairobi.

“Wanachohofu ni kitu gani, kwa nini wanaogopa uchunguzi, tunamwambia (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon) Sirro na Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) tunataka uchunguzi wa nje,” alisisitiza Mbowe

Michango ilivyotolewa

Mbowe pia alizungumzia gharama za matibabu tangu alipofika hospitalini Nairobi Septemba 7 hadi Oktoba 10 kuwa zimefikia Sh412.7 milioni ambazo zimepatikana kutoka kwa watu mbalimbali waliochangia, kikiwamo chama hicho.

“Gharama ni kubwa ila gharama si kitu hata siku moja, kikubwa ni uhai wa Lissu. Tunataka kumuona Lissu akirudi ulingoni tuendeleze harakati na niwaomba Watanzania wasichoke kuchangia kwa kuwa Lissu atarudi barabarani,” alisema.

Akizungumzia mchanganuo wa michango, Mbowe alisema wabunge wa Chadema wamechanga Sh48.4 milioni, wananchi wamechangia Sh24.2 milioni kupitia simu ya mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko.

“Watu mbalimbali wakiwemo wanachama wa Chadema wamechanga Sh90 milioni kupitia akaunti iliyofunguliwa benki ya CRDB. Watanzania walio nje ya nchi kupitia Go Fund Me wamechanga dola 29,000 za Kimarekani.”

Mbowe aliwashukuru Watanzania mbalimbali kwa kuhamasisha akiwataja baadhi kuwa ni mwanadada anayeishi Marekani, Mange Kimambi na mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu kwa kuhamasisha michango.

Alisema wafanyabiashara wakihamasishwa na mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema wamechanga dola 18,000 na amewaomba Watanzania waendelee kuwapigania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad