VIGOGO wawili wa Chuo cha Uhasibu (TIA) jijini Dar es Salaam, leo wamepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Shilingi bilioni moja.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leornad Swai, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Shaha Mussa Hanzuruni na Onesphory Ambangile Luhungu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, imedaiwa kuwa kati ya Januari Mosi 2012 na Desemba 30 2014, katika chuo hicho kilichopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa walitenda makosa hayo.
Imedaiwa, washtakiwa, walitumia vibaya madaraka yao kwa kutofuata taratibu za manunuzi katika ununuzi wa ardhi wa chuo hicho (TIA) kampasi uya Mwanza na kimsababishia Vedasto Lupungo kupata manufaa ya Sh.1,097,681,107/=
Katika shtaka la pili imedaiwa siku na mahali hapo washtakiwa hao kwa ridhaa zao na matendo yao waliisababishia TIA hasara ya Sh. 1,097,681,107/- kwa kutofuata sheria za manunuzi wakati wa kusaini mkataba wa ardhi wa eneo la TIA kampasi ya Mwanza.
Kwa kuwa DPP ameipa mamlaka mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi, washtakiwa walipata nafasi ya kujibu tuhuma hizo ambapo wote wamekana kutenda makosa hayo na mahakama ikawasomea masharti ya dhamana kwa kuwa kesi hiyo inadhaminika.
Akisoma masharti ya dhamana, Hakimu Simba amewataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaoweka bondi ya Sh. milioni 250 kila mmoja, pia amemtaka mdhamini mmoja kati ya hao kuweka mahakamani pesa taslimu, Sh. milioni 250 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha ambayo ipo ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha wametakiwa kuwasilisha pasipoti zao na kwamba hawaruhusiwi kusafiri nje ya mkoa huo bila ruhusa ya maandishi kutoka mahakamani.
Vigogo wa Chuo cha Uhasibu Wapandishwa Kizimbani kwa Kuisababishia Hasara Serikali ya Zaidi ya Bilioni Moja
1
October 11, 2017
Tags
Chukua bilioni 1 utoe milioni 250 na kesi kwishinei
ReplyDelete