Katika soka huwa kuna dirisha dogo la usajili ambalo linapofunguliwa, timu huchuana kusaka wachezaji.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa vyama vya siasa ambavyo vinajiweka sawa kuchuana kuwania kata 43 zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa utafanyika Novemba 26.
Uchaguzi huo unafanyika kutokana na nafasi hizo kuwa wazi baada ya madiwani waliokuwapo kufariki dunia, kutohudhuria vikao na wengine ushindi wao kutenguliwa mahakamani.
Katika maandalizi hayo, naibu katibu mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya alisema chama hicho kiliamua kujifungia kwa siku mbili mfululizo kujadili namna kitakavyoshiriki uchaguzi huo na kuibuka kidedea.
“Jana (juzi) baada ya NEC kutangaza uchaguzi viongozi tulikutana na kufanya kikao hadi saa sita usiku. Miongoni mwa mambo tuliyoyajadili ni pamoja na kupitia kata moja baada ya nyingine ili kujua nguvu ipo wapi ili tuweze kushiriki kwa asilimia 100.
“Tuliwasiliana pia na viongozi wa wilaya ili kujua uhai wa chama wakati wa kuelekea katika uchaguzi huu wa marudio,” alisema Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua, Tabora.
Sakaya ambaye yupo katika kundi la uongozi wa chama hicho linalomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, alisema kuna baadhi ya maeneo ambayo CUF itashiriki kwa asilimia 100 na mengine asilimia 50 kulingana na nguvu na kukubalika kwake.
Lakini Sakaya akisema hakutakuwa na ushirikiano miongoni mwa vyama vinavyounda Ukawa na kwamba kila chama kitasimama kivyake.
Kwa upande mwingine, Salim Bimani, mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma wa CUF unaompinga Profesa Lipumba, alikuwa na mtazamo tofauti akisema ushirikiano huo wa vyama vinne uliopewa jina la umoja wa katiba ya wananchi ndiyo utakaosaidia kuiangusha CCM.
“Kesho tutatoa taarifa rasmi kuhusu uchaguzi huu. Hata hivyo, nimesikia upande wa Profesa Ibrahim Lipumba hautaki ushirikiano, nawaambia hivi hawawezi kushinda hata kata moja endapo watasimama peke yao,” alisema Bimani.
Kuunga mkono hilo, naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema chama hicho kinatarajia kukutana wiki ijayo kupanga namna ya kushiriki uchaguzi huo kwa kushirikiana na wana Ukawa ambao ni CUF, NCCR-Mageuzi, NLD. “Huu uchaguzi siyo wa kawaida kutokana na hali halisi ilivyo... Nitawashangaa sana wale watakaotoka nyumbani kwao na kwenda kupigia kura CCM,” alisema Mwalimu.
Pia, katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda alisema maandalizi yalishaanza na yanaendelea kufanyika kwa kushirikiana na Ukawa ili kujua namna watakavyoweza kuachiana kata katika uchaguzi huo.
Wakati Sakaya na Ukawa wakisema hayo, katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema chama hicho, kimeshajipanga na hakina maneno yoyote ya kuzungumza.
“CCM imefanya kazi kubwa na ukweli unaonekana kupitia Serikali ya Awamu Tano na ukweli utadhihirika baada ya matokeo,” alisema Polepole.
Alisema wagombea wote watakaopitishwa ni wale wanaokubalika ndani ya CCM hadi kwa wananchi na wakishinda watakuwa viongozi na watumishi kwa watakaowaongoza.