Wachambuzi wa Masuala ya Kisiasa Watoa Sababu za Rais Magufuli Kurudia Rudia Mambo Katika Hotuba Zake

Wachambuzi wa Masuala ya Kisiasa Watoa Sababu za Rais Magufuli Kurudia Rudia Mambo Katika Hotuba Zake
Wakati Rais John Magufuli akitarajia kufikisha miaka miwili tangu alipoingia Ikulu Novemba 5 mwaka juzi, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameeleza sababu za kiongozi huyo kurudia rudia mambo katika kila hotuba anazozitoa.

Katika hotuba zake, Rais Magufuli mbali ya kuzungumzia mambo mengine, masuala ya watumishi hewa, vyeti feki, vita ya kiuchumi na mafisadi pamoja na mapambano dhidi ya dawa za kulevya amekuwa haachi kuyasemea.

Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti wamekuwa na mtazamo tofauti juu ya masuala hayo ambayo wameyaelezea kama ajenda yake kuelekea uchaguzi mkuu na wengine wakitaka asirudi nyuma, aendelee nayo.

Rais Magufuli, amekuwa akiyazungumzia masuala hayo huku akisisitiza Watanzania wazidi kumwombea kwa kuwa vita ya kiuchumi ni ngumu.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Onesmo Ole Ngurumwa alisema kiongozi yeyote anapenda kuzungumzia maeneo aliyoyafanya tofauti na wengine ili kuonyesha mafanikio yake.

“Suala la vyeti feki halikuweza kufanyika huko nyuma... rasilimali amejaribu kwa namna moja au nyingine lakini waliopita nao walifanya,” alisema Ole Ngurumwa

“Lakini Rais anapaswa kuangalia pia yale yanayopaswa kuendelezwa na anapotekeleza hayo anayoyafanya anapaswa kuyaingiza katika Katiba ili huko mbele tusije kupata vyeti feki, watumishi hewa au wezi wa rasilimali,” alisema.

Wakati Olengurumwa akisema hayo, mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alikuwa na mtazamo tofauti: “Nadhani ni mkakati wake kutumia maeneo hayo kama karata zake kwa uchaguzi wa 2020.”

Kafulila ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chadema alisema kwenye uchaguzi ujao yapo maeneo ambayo Rais Magufuli atayatumia kama karata yake na yapo maeneo upinzani utayatumia kutafuta dola.

Alisema maeneo hayo yatategemea mwenendo wa jumla wa hali ya siasa, uchumi na masuala mengine ya kijamii kufikia wakati huo.

“Inawezekana masuala ya vyeti feki, vita ya ufisadi, watumishi hewa yakawa ajenda za JPM 2020 wakati masuala ya demokrasia na mwenendo wa uchumi na biashara yakawa hoja za upinzani. Kila upande utatumia karata inayoweza kusaidia kuvuna ushindi kutegemea wakati huo hali itakuwaje,” alisema Kafulila.

Aliyekuwa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Dk Charles Kitima hakuwa mbali na Kafulila, alisema Rais Magufuli amekuwa akirudiarudia mambo hayo ambayo anayaona yalikuwa ni tatizo sugu hivyo anataka kuwathibitishia wapigakura wake jinsi anavyoyashughulikia.

Alisema ili kukabiliana nayo, “Lazima yatolewe elimu ya kutosha kwanza. Mfano tunataka Tanzania ya viwanda, hatujaelezwa viwanda vya aina gani, wananchi watachangia nini, wakulima watachangia nini,” alisema Dk Kitima.

Alisema hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitumia muda mwingine kuwaelimisha wananchi kupinga ubepari kwa kuhakikisha wanatambua jukumu lao, nchi inataka nini na wafanye nini na kwamba elimu ilisaidia kwa sehemu kubwa, “Nyerere alihakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa jambo na alipokuwa akianza utekelezaji kila mtu anajua wajibu wake na hiki ndicho tunakikosa kwa sasa na jukumu hilo si la Rais peke yake, hata wasaidizi wake kwenye wizara wanapaswa kumsaidia.”

Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega alisema masuala hayo ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakirudisha nchi nyuma kwa baadhi ya wachache kujinufaisha rasilimali za Taifa na kugeuzwa shamba la bibi.

Alisema Rais Magufuli anapaswa kutilia makazo masuala hayo ili nchi isije kurudi ilikotoka huku akisema hata yeye jimboni kwake amekuwa akizungumzia masuala hayo.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Njelu Kasaka alisema: “Unajua kwa sasa tunashindwa kutoa maoni yetu kwa mambo yanayoendelea, tunataka kujua kwanza hivi wanaposema mchochezi au huyu si mzalendo wanamaanisha nini.”

Kasaka aliyekuwa miongoni mwa wabunge 55 walioasisi Kundi la G55 lililotaka kuundwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993, alisema kuna mambo anayoyaona lakini anashindwa kuyazungumzia ahikofia kuitwa mchochezi, “Nchi lazima tuijenge pamoja, hakuna mtu ambaye ni ‘perfect’ lazima asikilize wengine wanasemaje…kwa sasa tuko ‘carefully’ tunaona nchi inavyokwenda tu. Tunataka kuona hii tafsiri ya uchochezi inachukua sura gani.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad