Mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba ligi kuu soka Tanzania bara raundi ya nane umemalizika jioni hii kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaa kwa sare ya bao 1-1.
Simba ambao walikuwa wageni kwenye mchezo huo ndio walianza kutikisa nyavu za wenyeji wao Yanga kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57 lililopatika baada ya Emanuel Okwi kugongeana vyema na Haruna Niyonzima kisha Kichuya kupachika bao hilo.
Yanga hawakutoka mchezoni baada ya bao hilo badala yake walifanya shambulizi la haraka haraka na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 60 kupitia kwa Obrey Chirwa ambaye aliitendea haki pasi ya Godfrey Mwashiuya iliyotokana na kazi nzuri ya Ibrahim Ajibu.
Baada ya hapo timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini hakuna timu ambayo ilifanikiwa kuongeza bao hivyo hadi mwisho wa mchezo timu hizo zimetoka sare ya 1-1, na kugawana alama moja moja.
Matokeo hayo sasa yanaiacha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara VPL msimu wa 2017/18 ikiwa na alama 16 sawa na Yanga na Azam FC ambazo pia zina alama 16 zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga.
Yanga inabaki kwenye nafasi ya pili huku Azam FC ikisogea hadi nafasi ya tatu baada ya jana kushinda dhidi ya Mbeya City na kuongoza ligi kwa muda. Mtibwa Sugar inayo nafasi ya kuongoza ligi endapo itashinda mchezo wake wa kesho dhidi ya Singida United ambapo hadi sasa ina alama 15 hivyo itafikisha alama 18.