Wagombea Wenye ‘Harufu’ ya Edward Lowassa Watoswa

Katika kile kinachonekana mzimu wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa bado haujatoweka ndani ya CCM, wagombea kadhaa wa nafasi za uenyekiti wa wilaya, ambao wanatuhumiwa kumuunga mkono, wameondolewa, Mwananchi imeelezwa.

Lowassa, mmoja wa watu walioonekana kuwa na nguvu kubwa ndani ya CCM, alijiondoa mwaka 2015 baada ya jina lake kutopitishwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho. Kuondoka kwake kulifuatiwa na wenyeviti wa mikoa, wilaya, wabunge, madiwani na wanachama waliomfuata Chadema.

Wakati wa uchaguzi, aliyepitishwa kugombea urais, John Magufuli alikuwa akilalamika kuwa kuna baadhi ya wanachama ambao wanaunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliokubaliana kumpitisha Lowassa kugombea urais.

Mwishoni mwa mwaka jana, Mkutano Mkuu wa CCM uliwatimua wanachama 12, wakiwamo wajumbe wa Kamati Kuu, wenyeviti wa mikoa na wilaya kwa madai ya kukisaliti chama hicho, hasa kutokana na kushirikiana na Ukawa.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Meru, Furahini Mungure aliwahi kukaririwa akisema kuwa nguvu ya Lowassa, aliyekuwa mgombea wa Chadema kupitia Ukawa ndiyo iliyompa ushindi mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari huku aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akisema waziri mkuu huyo alisumbua uchaguzi huo

Lakini fagio hilo halikumaliza vumbi aliloliacha mbunge huyo wa zamani wa Monduli na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Ikulu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita ilizingatia suala hilo katika mchujo wa wagombea uenyekiti.

Mbali na kigezo hicho, sera mpya ya kutaka mwanachama asiwe na nafasi mbili za utendaji pia ilitumika kuwaengua wagombea, sambamba na mambo mengine kama utumishi serikalini.

Orodha ya wagombea waliopitishwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho iliyotangazwa juzi katika gazeti la chama hicho, inaonyesha wengi wa wenyeviti hao waliomba kupata ridhaa kutetea nafasi zao lakini wameondolewa.

Orodha hiyo iliyojumuisha mikoa 33 ya Tanzania Bara na Zanzibar, inapeleka machungu kwa baadhi ya wenyeviti hao.

Mkoani Dar es Salaam, baadhi ya watu wanaotuhumiwa kumuunga mkono waziri huyo mkuu wa zamani, wameondolewa. Wenyeviti wa wilaya za Kinondoni na Ilala walikutwa na makosa ya usaliti na kuadhibiwa na chama hicho, hivyo hawakuwa na sifa za kugombea.

Mkoani Dodoma, wenyeviti wawili wameachwa ambao ni Paulo Luhamo kutoka Wilaya ya Dodoma Mjini na Philimon Mdate kutoka Bahi.

Kwa upande wa Geita, kati ya wenyeviti watano, ni mmoja pekee kutoka Wilaya ya Chato, Ibrahim Bagula aliyeachwa huku mgombea kutoka Mbogwe, Deus Lyamkando akipitishwa.

Mkoa wa Iringa, ambako kulikuwa na mgogoro mkubwa ndani ya CCM kuhusu wagombea urais, ndiyo ulioathirika zaidi kutokana na wenyeviti wake wote kukatwa majina yao na vikao hivyo vya juu vya chama.

Waliokatwa ni pamoja na (Abeid Kiponza (Iringa Mjini), Delfina Mtavialo (Iringa Vijijini), Seth Motto (Kilolo) na Yohanes Kaguo wa Mufindi.

Juhudi za Mwananchi kupata sababu za kuondolewa kwa wagombea hao hazikufanikiwa, lakini mkoa huo ulikuwa na vuguvugu kubwa la upinzani.

Kwa upande wa Kagera, kati ya wenyeviti watano, mgombea mmoja kutoka Bukoba Mjini, Yusuph Ngaiza amekatwa. Bukoba Mjini pia ni kati ya sehemu ambazo upinzani ulikuwa na nguvu.

Mkoani Kigoma, kati ya wenyeviti saba waliojitokeza kutetea nafasi zao, wawili wamekatwa ambao ni Kassim Kasambwe (Kigoma Mjini) na Almas Mohamed Kabambe (Uvinza).

Kilimanjaro, moja ya mikoa ambayo upinzani unashika majimbo mengi, wilaya zote zinatarajiwa kuwa na sura mpya kutokana na CCM kuagiza kurudiwa kwa uchaguzi katika wilaya tatu, huku wawili wakiamua kutogombea na jina la mmoja kutoka Same, Agustino Kessy, kukatwa.

Mkoani Mara kati ya wenyeviti sita, wawili hawajapitishwa ambao ni Chacha Gimanwa (Bunda) na Rashid Bugomba (Tarime). Mara pia ni ngome ya upinzani.

Mkoani Mbeya, wenyeviti watatu kati ya sita wameachwa. Wenyeviti hao ni Ephrahimu Mwaitenda (Mbeya Mjini), Ipyana Seme (Vijijini) na Mathayo Mwangomo (Mbarali).

Mkoani Morogoro, ambako CCM ina nguvu, kati ya wenyeviti wanane, Bassor Udulete kutoka Kilosa ambaye anadaiwa kushiriki kusaliti chama hicho, ameondolewa.

Katika Mkoa wa Mtwara, wagombea watatu; Ally Chimkawene (Mtwara Mjini), Ally Kombo (Vijijini), Abdu Namtula (Tandahimba) na Kazumari Mlilo (Masasi) wameachwa.

Waliokatwa mkoani Mwanza ni pamoja na mwenyekiti wa Wilaya ya Sengerema, Chasama Kamata na wa Misungwi, Judith Mlolwa wakati mkoani Njombe, CCM imeagiza mchakato uanze upya wilayani Makete.

Waliokatwa mkoani Pwani ambako kuna wilaya nane ni Hamisi Kanesa (Kibaha Vijijini na Omary Kubwa (Mkuranga) wakati Shinyanga hakuna mgombea aliyeachwa isipokuwa kwa mwenyekiti wa Wilaya ya Kahama, Mabara Mlolwa, ambaye hakugombea.

Hali ni kama hiyo mkoani Arusha ambako mgombea mmoja, Mustapha Mbwambo (Karatu) amekatwa, lakini wengine hawakugombea kutokana na baadhi kufukuzwa na wengine kuzuiwa na kanuni inayokataza kushika nafasi mbili.

Katika wilaya sita za Mkoa wa Singida, walioachwa ni watatu ambao ni Hassan Tati (Ikungi), Barnabas Hanje (Singida Vijijini) na Hamad Hamad (Manyoni), huku aliyekuwa mwenyekiti wa Manispaa ya Singida, Hamisi Nguli akishindwa kugombea kutokana na kufukuzwa na NEC.

Mkoani Tabora, wenyeviti wawili hawakugombea; Mussa Ntimizi ambaye ni mbunge na Seleman Mbogo (Sikonge), huku Costa Olomi (Igunga) na Moshi Abdallahman wa Tabora Mjini wakienguliwa.

Mkoani Tanga ni mwenyekiti mmoja pekee kutoka Wilaya ya Tanga, Kassim Mbuguni ambaye jina lake limekatwa.

Kwa upande wa visiwani Zanzibar katika Mkoa wa Kaskazini Pemba kati ya wenyeviti 12, walikatwa ni watatu pekee ambao ni wa Micheweni (Khamis Hamad Yussuf), Chakechake (Yussuf Ali Juma) pamoja na wa Mfenesini, Mjumbe Msuri Mjumbe.

Aliyekatwa azungumza

Mmoja wa wenyeviti hao ambao jina lake limekatwa amesema hana kinyongo na uamuzi huo.

Alisema kilichofanyika ni kwa mujibu wa kanuni na taratibu cha chama hicho na kwamba hana nia ya kukata rufaa.

“Matokeo hayo nimeyapokea kwa moyo mkunjufu na sioni haja ya kukata rufaa,” alisema Ephrahim Mwaitenda wa Mbeya Mjini.

“Nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu katika kukitumia chama changu. Inawezekana chama kimeona ni vyema nipumzike kwa kuwa siwezi kuendana kasi wanayoitaka kwa sasa.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad