Matokeo ya uchaguzi wa Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yamepingwa katika wilaya nne kati ya saba za Mkoa wa Mwanza kutokana na madai ya kugubikwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Acheny Maulid alitaja wilaya ambazo matokeo yake yamewekewa pingamizi kuwa ni Magu, Nyamagana, Misungwi na Sengerema.
Aliwataja wenyeviti ambao ushindi wao unapingwa ni Zebedayo Athumani kutoka Nyamagana, Daudi Gambadu (Misungwi), Zabloni Makoye (Magu) na Agostine Makoye wa Sengerema.
“Vikao husika vitakutana kujadili na kuamua pingamizi hizo kwa mujibu wa katiba na kanuni za uchaguzi ndani ya chama,” alisema Maulid.
Uchaguzi wa wenyeviti wa wilaya wa CCM katika wilaya zote saba za Mkoa wa Mwanza ulifanyika Oktoba 5. Wenyeviti wengine waliochaguliwa ambao hawajawekewa pingamizi hadi juzi ni Peter Muyanga kutoka Kwimba, Ally Mambile (Ukerewe) na Nelson Mesha wa Ilemela.