Wanachama wa CCM Wampinga Polepole Sakata la Ubunge, Madiwani

Wanachama wa CCM Wampinga Polepole Sakata la  Ubunge, Madiwani
Wakati katibu wa oganaizesheni wa CCM, Pereira Silima akikanusha kupitishwa kwa sharti la ukazi kwa wagombea udiwani na ubunge, chama hicho kimewataka watumishi wa umma walioshinda uchaguzi katika ngazi ya wilaya kuamua moja; ajira au siasa.
Juzi, katibu wa uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema katika kipindi cha redio cha Times FM kuwa wanaogombea udiwani na ubunge mwaka 2020 watatakiwa kuwa wakazi wa maeneo wanayogombea, lakini mara moja akapata maswali kutoka kwa wanachama.
Lakini jana, Silima alisema CCM haiwezi kuweka sharti hilo kwa kuwa linakiuka Ibara ya 67 (1 a-c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inaeleza sifa za mtu ambaye hatakuwa na sifa za kugombea, hali kadhalika Sheria za Uchaguzi.
“Nikiwa katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa mwenye dhamana ya uchaguzi, napenda kuwajulisha kwamba Chama cha Mapinduzi kimefanya mabadiliko katika katiba yake,” anasema Silima.
“Mabadiliko ambayo yamepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika 12/03/2017, pamoja na kanuni za uchaguzi wa chama na hakuna mahali popote palipoandikwa kuwa wagombea wa udiwani na ubunge watajadiliwa kwa sifa ya kuishi jimboni.”
Silima amewataka wanachama kuzipuuza habari hizo.
Katika hatua nyingine, makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula amewataka watumishi waliogombea na kushinda nafasi za uenyekiti na ujumbe wa wilaya, kuchagua moja; ajira au uongozi.
Katika toleo la juzi la Uhuru, gazeti la chama hicho tawala, Mangula amekaririwa akisema CCM itawashughulikia watendaji wake pamoja na watu ambao walikiuka maelekezo ya waraka unaozuia watendaji wa Serikali kuwania uongozi ndani ya chama.
Mangula alisema baadhi ya wilaya na mikoa ilikiuka kwa makusudi waraka huo kwa kutoa tafsiri potofu kama vile kueleza nafasi zilizozuiwa ni za utendaji, jambo ambalo alidai si kweli.
Mangula amekaririwa akisema waraka huo umeeleza bayana kwamba watumishi wa Serikali hawaruhusiwi kuwania uongozi ndani ya chama. Alisema katika hali ya kushangaza, baadhi ya watendaji kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa vikao vya uteuzi, wamewapitisha na wengine wameshinda nafasi mbalimbali.
Alisema CCM inaliona hilo kama tukio la uvunjaji wa kanuni za maadili ya uongozi na hivyo inawataka wahusika kuanza kuwajibika kabla ya kusubiri uamuzi wa vikao vya juu.
Mangula alisema chama kinaweza kuchukua uamuzi wa kufuta matokeo ya uchaguzi katika baadhi ya wilaya kitakapojiridhisha kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni kwa kuwa suala la rushwa ni kinyume na maadili ya viongozi wa CCM.
Watumishi wa umma walioshinda
Wanachama waliotangazwa kushinda ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM ni wakuu wa mikoa ya Mtwara, Halima Dendego na Morogoro, Dk Kebwe Stephen.
Wakuu wa wilaya waliogombea uongozi ndani ya CCM na kushinda ni Simon Odunga (Chemba), Christina Mndeme (Dodoma) na Elizabeth Kitundu (Bai) mkoani Dodoma.
Mkoani Morogoro, wakuu wa wilaya waliogombea na kushinda ni Alhaji Mohamed Utaly (Mvomero) na Seriel Nchembe (Gairo).
Wakuu wa wilaya wengine walioshinda ni Raymond Mushi (Babati, Manyara), Herman Kapufi (Geita), Kaul Kiteleki (katibu tarafa wa Makuyuni, Arusha), Alexander Mnyeti (mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Arusha), Salum Palango (katibu tawala wa Nanyumbu, ambaye alishinda ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM.
Wengine ni Salvatory Richard (mtumishi Idara ya Elimu, Mvomero) na dereva wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Wengine walioshinda nafasi ya ujumbe ni Elishilia Kaaya ambaye ni mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Dk Daniel Mrisho.
Katika hatua nyingine, CCM mkoani Morogoro imesema inasubiri maelekezo ya uongozi wa Taifa kuwafyeka watumishi wa umma walioshiriki uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.
Katibu wa mkoa, Kulwa Milonge amesema chama hicho hakitasita kuwachukulia hatua wanachama wake ambao ni watumishi wa umma waliochaguliwa katika nafasi za uongozi ndani ya chama iwapo wataelekezwa kufanya hivyo na uongozi wa Taifa wa CCM
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad