Wanafunzi watano na mlinzi mmoja wamepigwa risasi na kuuawa katika shambulio la asubuhi katika shule moja ya upili Kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka wa Sudan Kusini.
Mashahidi wanasema watu watatu waliokuwa na silaha, mmoja wao akiwa mwanafunzi wa zamani walivamia mabweni katika Shule ya Upili ya Lokichogio leo asubuhi.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo anasema kuwa mshambulizi mkuu alikuwa mwanafunzi wa zamani katika shule hiyo aliyefukuzwa kwenda shuleni baada kupigana na mwenzake.
Aliagizwa kurudi na wazazi wake lakini hakufanya hivyo.
Walioshuhudia walisema kuwa mwanafunzi huyo alirudi shuleni usiku wa manane na wenzake wawili.
Inadaiwa kuwa walimpiga risasi na kumuua mlinzi na kisha kwenda katika mabweni wakimtafuta mwanafunzi waliyepigana naye awali.
Mwanafunzi huyo hakuwa shuleni wakati huo na washambuliaji hao waliwapiga risasi na kuwaua wanafunzi watano na kuwabaka wasichana wawili.
Chama cha msalaba mwekundu kimesema kuwa kimewahamisha waliojeruhiwa hadi hospitalini.
Lokochogio iko karibu na mpaka wa Sudan Kusini na Ethiopia na wakaazi wengi wa eneo hilo hubeba bunduki na ni wachungaji wanaolinda mifugo wao dhidi ya wizi.