“Hakuna ngono hadi baada ya uchaguzi” ni kauli ya hamasa iliyoanzishwa na mgombea urais kwa tiketi ya Nasa, Raila Odinga kwamba wakati wa vita wanaume huwa hawalali na wake zao. Kauli hiyo ilikuwa maarufu kipindi cha kuelekea uchaguzi wa Agosti 8.
“Agosti 8 inakuja; itakuwa siku ya kihistoria na hakuna mtu atakayeachwa bila kupiga kura. Wanaume watalala nje. Siku itakapofika, hakuna mwanamume kulala na mkewe,” alikuwa akisema.
“Mnapokwenda vitani, ngono ni mkosi,” Odinga alinukuriwa akisema Juni
Safari hii kikundi cha wanawake nchini kimetoa rai ngono ipigwe marufuku kuelekea uchaguzi mkuu wa marudio ambao umeamriwa na Mahakama ya Juu.
Ingawa sintofahamu imetawala uchaguzi huo uliopangwa Oktoba 26, wanawake katika mji wa Nyeri katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano walisema hawatashiriki ngono na waume zao hadi Uhuru Kenyatta atakapoapishwa kuwa rais kwa muhula wa pili.
Kiongozi wa kikundi hicho, Rahab Mukami, ambaye ni mwakilishi wa wanawake alisema wanawake wameimarisha kampeni kuhakikisha Kenyatta anashinda.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesisitiza kwamba uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa licha ya mgomo ulioitishwa na Odinga wa National Super Alliance (Nasa).
Nasa wametoa wito kwa wafuasi wao kufanya maandamano makubwa siku ya uchaguzi. Mara kadhaa wafuasi wao wamepambana na polisi katika mitaa ambayo muungano huo ni ngome zao.