Wapinzani Wazungumzia Mikutano ya Hadhara Wakiwa Ikulu

Wapinzani Wazungumzia Mikutano ya Hadhara Wakiwa Ikulu
Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba jana waliibua suala la mikutano ya hadhara wakati walipopewa nafasi ya kuzungumza katika hafla ya Rais iliyofanyika Ikulu.

Wote wawili walitaja “mikutano ya hadhara” wakati walipokuwa wakikamilisha ushauri wao mfupi wakati wa hafla ya kutunuku wajumbe wa kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini unaosafirishwa nje, biashara, sheria na mikataba ya madini.

Wakati Profesa Lipumba alisema ametumia nafasi hiyo kutoa yake kwa kuwa mikutano ya hadhara imezuiwa, Cheyo alisema hawezi kuzungumza mengi kuepuka kuonekana amegeuza fursa hiyo kuwa mkutano wa hadhara.

Cheyo alijirudi baada ya kutumia muda mrefu zaidi ya Profesa Lipumba, akijikita katika kueleza kilio cha muda mrefu cha kutaka Serikali ifungue macho na kuchukua hatua ili rasilimali za nchi ziweze kusaidia Watanzania.

“Kuna siku moja nilikuwa , nikawaambia wazungu tumechoka kuitwa masikini. Huwezi ukawa masikini wakati una gesi ya ujazo wa 57 trilioni, na madini na kila kitu, halafu unaitwa masikini. Tumechoka,” alisema Cheyo.

“Wewe (Rais) umetusaidia kuondoka katika kuchoka huku. Asante sana Mheshimiwa Rais.”

Cheyo alitumia nafasi hiyo kumuomba Rais awaamini Watanzania kwa kuwa nchi ina watu wengi wenye akili.

“Tanzania ina watu wenye bongo, na ndio maana inaitwa Bongoland,” alisema huku akishangiliwa.

Hata hivyo aligeukia suala la siasa akitaka vyama visigeuze iviepuke vurugu.

“Nawaomba rafiki zangu ambao tuko katika vyama vya ushindani, hesbu tusigeuze mfumo huu wa vyama vingi kuwa kiwanda cha chuki,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Bariadi Mashariki.

“Mwalimu (Julius Nyerere) aliyefanya kila nguvu kuwaambia wana-CCM-- pamoja na asilimia 20 kusema tuwe na vyama vingi- tuwe na vyama vingi.

“Nia yake haikuwa kutengeneza kiwanda cha kutukanana, kiwanda cha chuki, kiwanda cha kukosa uzalendo. Vyama vya siasa tuwe kiungo cha Watanzania wote kushirikiana na uongozi ambao umechaguliwa kidemokrasia, kuongoza nchi yetu kwa sababu nchi hii itaendeshwa na sisi wote. Na wote tuna nafasi.”

Naye Profesa Lipumba alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais kwa kulipa kipa umbele suala la madini ambalo wamekuwa wakilipigia kelele.

“Sisi viongozi wa vyama vya siasa, hususan vyama vya upinzani, kwa muda mrefu, kwa miaka mingi, hasa kutokea mwaka 2000, tumepiga kelele sana kuhusu mikataba ya madini na namna maliasili zinavyoibiwa,” alisema.

Alisema itakuwa ajabu sasa wakianza kubeza juhudi hizo.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kabisa siasa za baadhi ya vyama vya upizani na wafuasi wao Tanzania zinaboa sana aisee. Wazungu wanakitu wanaita healing process yaani wakati wa kutibu majeraha yaliyosababishwa na mapambano baada uchaguzi mkuu wa nchi katika kutafuta viongozi wa kuingoza nchi. Katika kipindi hiki kwenye nchi za wenzetu ambao wana uweledi mzuri wa kutambua nini maana ya siasa na ushindani wake huwa ni kipindi cha kuwarejesha watu wao kuwa kitu kimoja tena na kushirikiana na serikali iliyochaguliwa ili kuijenga nchi yao. Lakini kwa wenye kufuatilia siasa za Tanzania utakumbuka siku ya kwanza raisi mteule John pombe Maghuful alipokwenda kukutana na viongozi wa siasa bungeni wapinzani walianza kuzomea na kumzomea muheshimiwa raisi hadi kupelekea wapinzani kutoka bungeni mbele ya wageni waalikwa wakiwemo wa mataifa ya nje wakati muheshimiwa raisi akihutubia. Kitendo kile kilicho fanywa wakati ule na upinzani kilikuwa ni aibu kubwa kwa taifa na nchi yetu. Na ni wao wenyewe wapinzani ndio waliojijengea na kujenga misingi ghasi ya siasa za chuki wanazoendelea nazo hadi hivi tunavyozungumza. Huwezi kumlaumu muheshiwa raisi na serikali yake hata kidogo kwa hatua anazozichukuwa kuwazibiti wapinzani kwani ni wao wenyewe ndio walio muelekeza jinsi gani ya kudili nao. Sasa unashangaa sana unaposikia wapinzani wanapiga kelele wanaonewa. Na wameshangaika sana mpaka nchi za nje kutafuta sapoti za nchi zenye nguvu duniani ili kumuazibu Maghuful na serikali yake kwa madai ya wapinzani kuminywa demokrasia lakini wamegonga ukuta. Nadhani wapinzani wa siasa na viongozi wao ni vichwa maji labda wamesahau. Wazungu kuna msemo wanasema..First impression is the lasting impression. Ughasi ule na kejeli za dharau waliouonesha wapinzani wa siasa siku ya kwanza walipokutana na Maghuful pale bungeni ndio picha halisi aliondoka nao muheshimiwa raisi kuelekea katika safari yake ya uraisi. Na ni ushahidi tosha kabisa wa kuuwasilisha kwa mataifa ya kigeni wakati wowote wapinzani watakapo lalamika kuwa wanaonea kisiasa .Maghuful na serikaliyake wanaweza kuyaambia mataifa ya kigeni yakwamba hawa watu walishanipinga mimi kabla hata sijaanza kazi wakati nikiwa raisi wa kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kanisa ni watu wa kuwapuuza na hata ushahidi wa video ninao. Kwa hivyo utaona jinsi gani wapinzani wa siasa Tanzania wanavyokosa maono ya mbali kiasi cha kuja kujiumiza wao wenyewe wakiilalamikia serikali kuwaumiza.

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad