Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira amewafikisha watendaji watano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kwenye vyombo vya uchunguzi.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo alilopewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyomtaka kuwafikisha watendaji hao kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Akizungumza na gazeti hili jana ikiwa ni siku ya mwisho ya agizo hilo, Jenerali Rwegasira alisema: “Nimepeleka huko kama nilivyotakiwa, kazi yangu ya kutekeleza maagizo hayo nimefanya.”
Wakati Rwegasira akiwafikisha katika vyombo hivyo vya uchunguzi, ameshauriwa kujiuzulu kufuatia ubadhirifu wa mabilioni ya fedha yaliyofanywa na taasisi anazozisimamia.
Taasisi hizo ambazo Jenerali Rwegasira ni ofisa masurufu ambazo ziliitwa na kamati hiyo kwa ajili ya mahojiano kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini madudu hayo ni; Polisi, Idara ya Uhamiaji na Nida.
Jenerali Rwegasira na maofisa wa idara hizo kwa siku tatu mfululizo wamekuwa katika kiti moto mbele ya PAC ambayo inapitia ripoti ya mwaka 2015/16 kwa taasisi hizo.
Ashauriwa kujiuzulu
Akichangia hoja katika kamati hiyo jana Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alimshauri Jenerali Rwegasira kuomba kuondolewa kwa kuwa uchafu huo utamharibia sifa aliyoijenga kwa miaka mingi.
Mbunge huyo alisema Jenerali Rwegasira amefanya kazi kubwa kwenye nchi tena ya kutukuka, ni vyema kukabidhi kazi yake kwa Rais kama watu wa taasisi hizo wasipojirekebisha. “Haya madudu matatu ya Nida, Polisi na Uhamiaji yanaweza kukuchafulia sifa yako kwa sababu vitu vinavyofanywa huko nje si rahisi kwa Katibu mkuu kujua.”
Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula alisema Katibu mkuu amefanya kazi iliyotukuka kuna mambo hayaendi vizuri na kwamba si yeye anayesababisha lakini baadhi ya watendaji wa chini yake ni tatizo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema majibu yaliyotolewa kwenye hoja za ukaguzi wa fungu hilo ni hafifu.
“Fedha inayozungumziwa ni mabilioni yametumika vibaya na kwa uzembe, inaonyesha Polisi kumekuwa na uzembe wa hali ya juu kuna watu wamejiwekea wigo… hawa waliostaafu si ajabu wameacha mizizi ambayo ndiyo inayotufikisha hapa,” alisema.
Kwa upande wake Jenerali Rwegasira alisema wameona kuna upungufu mkubwa na katika kujibu hoja wameonekana hawakidhi kiu ya wajumbe.
“Tunakwenda kuyafanyia kazi haya na maelekezo yaliyotolewa hapa ukweli unaonekana, tutakwenda kuelezana ukweli na kutekeleza maagizo haya na tutachukua hatua kadri tulivyoona,” alisema.