Watu watano wanaodaiwa kuwa ni wahalifu wameuawa katika eneo la Toangoma jijini Dar es Salaam, katika majibizano ya risasi na Polisi yaliyotokea usiku wa kuamkia leo Ijumaa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula amesema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna njama za uhalifu zimepangwa kufanyika maeneo hayo usiku wa jana, hivyo wakajipanga kwa ajili ya kudhibiti.
Amesema ilipofika muda walioambiwa kweli wahalifu hao ambao idadi yao haikuweza kupatikana, lakini walikuwa wengi, wakafika eneo la tukio na kupambana na polisi.
“Majibizano ya silaha yalikuwa makubwa kwa sababu walikuwa na silaha nzito, lakini Jeshi la Polisi lilijipanga imara kuwadhibiti na kufanikiwa kuua watano na wengine wakatokomea kusikojulikana,” amesema.
Amesema wananchi wasiwe na hofu na waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kunusuru usalama wao na mali zao.
“Tumejipanga na tunapopata taarifa za uhalifu, pamoja na askari wetu kuwa doria maeneo hayo, lakini hujipanga upya kwa ajili ya kupambana na tukio husika.”