Watumishi na madiwani wameingia kwenye mgogoro na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Nchembe kutokana na hatua yake ya kuwaweka rumande.
Hatua hiyo imesababisha baadhi ya watumishi na madiwani kuiomba Serikali kuchukua hatua kutatua mgogoro huo wa utendaji.
Nchembe anatuhumiwa kuagiza kukamatwa na kuwekwa ndani Diwani wa Msingisi, Stephano Mganga baada ya wananchi kupasua bomba na kuchota maji kwa ajili ya kuyauza.
Ilielezwa kuwa mkuu wa wilaya aliamuru diwani huyo kukamatwa kwa kushindwa kudhibiti tatizo hilo, lakini baada ya kuhojiwa aliachiwa.
Mganga alisema alikamatwa kwa agizo la mkuu wa wilaya akidaiwa kuchochea wananchi wasitoe mchango wa Mwenge.
Pia, Mganga alisema tayari ameitwa mara ya tatu polisi kuhojiwa kuhusu kutoa maelekezo ya ratiba ya mgawo wa maji tofauti na aliyotoa mkuu wa wilaya.
Alisema ratiba waliyojipangia ni kupata maji kila baada ya saa mbili, lakini mkuu wa wilaya aliagiza badala ya muda huo wapate kwa saa sita jambo ambalo diwani huyo hakuliafiki kwa kuwa lingesababisha wananchi wengine kukosa huduma.
“Mara zote tatu nilizohojiwa na kuachiwa ni kwa busara za mkuu wa kituo cha polisi, kwa kuwa DC alitaka nilazwe rumande,” alisema.
Mwingine ambaye ameonja ‘kibano’ cha mkuu wa wilaya ni Meneja wa Maji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Gairo, Herman Mundo aliyewekwa rumande kwa saa 13 kutokana na majibu yake ya barua kwa Nchembe.
Mundo alisema alipokea barua ya mkuu wa wilaya ikimtaka aongeze muda wa mgawo wa maji kutoka saa mbili hadi sita kwa siku.
“Nilipokea barua hiyo nikamjibu kitaalamu kwamba suala hilo ni gumu kwa kuwa maji yanayopatikana ni kidogo ndiyo maana tunagawa kwa saa mbili, lakini baada ya kupokea barua alisema nimemjibu jeuri, nilikamatwa na kuwekwa ndani,” alisema.
Alikamatwa Agosti 6 na kushikiliwa kwa saa tatu kabla ya kuachiwa ili akahudhurie mkutano wa wahandisi ulioitishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (Moruwasa).
Mundo alisema aliporejea hakuripoti polisi, Agosti 11 alikamatwa ili kukamilisha muda wa saa 48 kama ilivyokuwa imeagizwa na mkuu wa wilaya.
Alisema alishikiliwa saa tatu asubuhi na kuachiwa saa tano usiku kutokana na agizo kutoka mamlaka za juu.
Orodha ya walioonja joto
Wengine waliowekwa ndani na kulala siku moja ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magoeko, Daudi Mbena (40) kutokana na kutoitisha mikutano ya kitongoji.
Pia, mwandishi wa Mbena wa mihtasari ya vikao vya wananchi, Chitemo (61).
Kauli ya DC, mkurugenzi
Nchembe alisema aliagiza Mbena na Chitemo wawekwe ndani ili kuwanusuru wasipigwe na wananchi kwenye mkutano.
“Siku hiyo nilikwenda kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa ili kutatua mgogoro kati ya wananchi na mwenyekiti huyo, vurugu zilipotokea wananchi wakisema hawamtaki na walitaka kuwapiga nikaita polisi wakawachukua,” alisema.
Kuhusu tuhuma za madiwani na watumishi wengine wa halmashauri, Nchembe alisema zimeshaundwa kamati za kufuatilia migogoro hiyo, hivyo hawezi kuzizungumzia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Agnes Mkandya hakuwa tayari kuzungumzia hilo kwa madai kuwa imeundwa kamati.
“Jamani hatuwezi kuzungumzia tena haya mambo kwenye vyombo vya habari, ebu tuacheni tayari kamati ilishatuhoji,” alisema Mkandya.
Matokeo ya kamati
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rachel Nyangasi aliziomba mamlaka kuwapatia taarifa ili waweze kuzifanyia kazi. “Tumehojiwa na kamati mbili zilizoundwa na Serikali kufuatilia mgogoro huo, tunaomba zilete majibu kama tunatakiwa tujirekebishe tufanye hivyo ili mambo yaende,” alisema.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari alisema kuwa tayari kamati zimekamilisha kazi na ripoti zimeshawasilishwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Hivi karibuni Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby alimuomba aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi (Tamisemi), Suleiman Jafo kutatua mgogoro uliopo kati ya mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri na baadhi ya wakuu wa idara.