Kwa wanamichezo kuna msemo maarufu kwamba makocha wanaajiriwa ili kufukuzwa na kuna wakati wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini walizitazama wizara mbili; Maliasili na Utalii na ile ya Nishati na Madini katika sura hiyo.
Katika kipindi cha miaka 12, Maliasili na Utalii imeongozwa na mawaziri saba huku Nishati na Madini wakiwa sita kuanzia mwaka 2005 kabla ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri lililofanywa mwishoni mwa wiki na Rais John Magufuli.
Mabadiliko hayo ya mara kwa mara ikilinganishwa na wizara nyingine na sababu za kufanyika kwake ndiyo ambayo yamekuwa yakiibua maswali ya iwapo walioteuliwa watavuka salama pasi na kutumbukia kwenye tanuri la kashfa ambalo limewakumba wengi wa watangulizi wao katika wizara hizo.
Hata mabadiliko yaliyotangazwa na Rais Magufuli Jumamosi iliyopita yalitokana na kutenguliwa kwa uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (Tamisemi) na Edwin Ngonyani (Naibu Waziri wa Ujenzi).
Sababu za kutenguliwa kwa nyadhifa zao ni pamoja na ripoti za uchunguzi wa usafirishaji mchanga wa madini nje ya nchi, uendeshaji, usimamizi na udhibiti wa almasi na Tanzanite kubainisha ubovu wa mikataba, udhaifu wa sheria katika uendeshaji wa biashara ya madini.
Katika mabadiliko hayo makubwa ya kwanza kufanya na Rais Magufuli tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, ameigawa wizara hiyo na sasa Nishati inasimama yenyewe kama ilivyo kwa Madini.
Dk Medard Kalemani, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ambayo pia imekuwa ikikumbwa na kashfa za mara kwa mara kutokana na mikataba mibovu na tata ya umeme kama ya uingiaji mkataba mbovu wa uzalishaji umeme wa IPTL, Richmond, ndiye aliyepewa jukumu la kusimamia Nishati huku Angela Kairuki akikabidhiwa Wizara ya Madini.
Uteuzi wa Dk Kalemani katika wizara hiyo kumeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii ambako kwa ujumla, hoja kubwa imekuwa ni jinsi alivyoepuka mishale na kupanda hadi kileleni katika wizara hiyo.
Mjadala huo unatokana na ukweli kwamba mbunge huyo wa Chato, aliyeingia bungeni akichukua nafasi ya Dk Magufuli, amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali katika Wizara ya Nishati na Madini ikiwamo ya mkurugenzi wa sheria.
Katika mijadala hiyo, wapo waliogusia pia kuwa huenda Rais amejiridhisha kuwa hahusiki na makandokando ya mikataba mibovu iliyoisababishia hasara Taifa ambayo imewakumba mawaziri na vigogo wengi katika wizara hiyo.
Lakini wapo wanaoiangalia hoja hiyo kwa mtazamo tofauti, wakisema kuwapo kwake wizarani hapo kwa muda mrefu akiwa mwanasheria na baadaye mkurugenzi, hakuwezi kumuacha salama dhidi ya ubovu wa mikataba inayoibuliwa hivi sasa.
Madai hayo yameshikiwa bango na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa akisema Dk Kalemani alikuwapo katika kipindi chote ambacho wizara hiyo ilikuwa ikikumbwa na kashfa mbalimbali zikiwamo za mikataba mibovu, “Unawezaje kumtofautisha mkurugenzi wa sheria na mikataba mibovu ambayo sasa imeiingiza nchi katika sitofahamu?
Mwaka 1999, Kalemani alifanya kazi katika Wizara ya Nishati na Madini akiwa ofisa mwandamizi wa sheria mpaka mwaka 2006. Baadaye mwaka 2013 hadi 2015, alikuwa mkurugenzi wa sheria.
Hata hivyo, waziri mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Njelu Kasaka alitofautiana na Msigwa akisema bila shaka Rais amejiridhisha kuhusu usafi wa waziri huyo.
“Unajua Rais ana macho mengi, pia ana njia nyingi za kujua mtumishi yupi ni msafi au amechafuka. Ukiwa nje huwezi kujua nani kachafuka lakini yeye ana uwezo wa kupata taarifa endapo mtumishi huyo alijiingiza moja kwa moja katika uchafu au wakati wanafanya uchafu huo yeye alijitenga pembeni.
Alisema anaamini kuwa Rais amejiridhisha na Dk Kalemani kwamba alikuwa msafi na kusisitiza kwamba aachwe afanye kazi aliyoagizwa.
Kasaka pia alimpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kuigawa wizara hiyo na kusema endapo waziri aliyepewa jukumu la kuiongoza akiitendea haki, italeta mafanikio.
“Hii wizara ilikuwa kubwa sana nishati pekee ina mambo mengi ilihitaji kugawanywa muda mrefu hata hivyo, hatujachelewa jambo la msingi ni kufanya kazi kwa lengo la kuleta maendeleo,” alisema.