Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema ana mpango wa kupeleka bungeni maombi ya kuongezwa muda wa kustaafu maprofesa.
Amesema umri wa kustaafu kwa sheria unawafanya wasomi hao washindwe kutumika vizuri kulijenga Taifa, hivyo ataomba wastaafu wakiwa na umri wa miaka 65 badala ya 55.
Mkuchika amesema hayo leo Jumatatu Oktoba 16, alipotembelea ofisi za Sekretarieti ya Ajira na kukutana na watendaji wa taasisi hiyo.
Amesema baadhi ya kada ambazo zinafanyiwa kazi na maprofesa zinatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.
Waziri amesema wengi wanapata uprofesa wakiwa na miaka 55 na hufanya kazi kwa miaka michache na kutakiwa kustaafu.
"Tutapeleka bungeni maombi kuwe na mabadiliko kidogo katika baadhi ya maeneo, hawa maprofesa wengi wanaofikia hatua hiyo wanakuwa na miaka kuanzia 50 na kuendelea halafu anafanya kazi kidogo anatakiwa kustaafu," amesema.
Amesema haitakuwa na maana kama wasomi hao wanatumia rasilimali za Taifa kufikia hatua hiyo halafu baada ya kuhitimu wanafanya kazi kwa muda mfupi na kutakiwa kustaafu.
Mkuchika amesema pia atawasilisha maeneo mengine ambayo yana upungufu unaotokana na sheria.
Amesema hayo akijibu changamoto iliyotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Xavier Daudi ambaye ameeleza kuwa sheria inatoa mwanya kwa taasisi nyingine za umma kuajiri bila kupitia sekretarieti hiyo.
"Kuna mgongano wa kisheria kati ya sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira na baadhi ya taasisi za umma ambazo nazo zina mamlaka ya kuajiri watumishi kwenye taasisi zao," amesema Daudi.
Akijibu hilo, Mkuchika amesema, "Naahidi katika kipindi changu cha uwaziri nitafanyia kazi changamoto hiyo na ikiwezekana maeneo yote yawekwe sawa kisheria."
Mkuchika amewaasa watendaji wa taasisi hiyo kujiweka mbali na vitendo vya rushwa.
"Fanyeni kazi bila upendeleo, jiwekeni mbali na rushwa natambua hakuna sehemu yenye changamoto ya rushwa kama Sekretarieti ya Ajira. Usiombe faili lako lije kwangu eti mfanyakazi wa sekretarieti ya ajira ana kesi ya rushwa," amesema.
Waziri amesema, "Nitasimamia utendaji wa watumishi wa umma, tufanye kazi kulingana na malipo tunayolipwa na kodi za Watanzania. Nafahamu wapo watumishi wa umma ambao wanalipwa mshahara ilhali hawafanyi kazi inavyostahili."
Kuhusu watumishi wa umma walioshiriki na kushinda katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema watawashughulikia kulingana na mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.
Amesema wakati nchi inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa mwongozo ambao ulielekeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma kulingana na nafasi zao wapo wanaoruhusiwa na wasioruhusiwa kushiriki kwenye siasa.