Weah Aendelea Kuongoza Matoko ya Uchaguzi
0
October 14, 2017
Mwanasoka nyota wa zamani wa kimataifa wa Liberia, Seneta George Weah bado ameendelea kuongoza matokeo ya urais yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jana Ijumaa huku Makamu wa Rais Joseph Boakai akimfuatia kwa karibu.
Baada ya theluthi moja ya kura kuhesabiwa kutoka katika vituo vya kupigia kura zaidi ya 5,000, Weah amejikusanyia asilimia 39.6 huku Boakai wa chama tawala cha Unity Party (UP) akipata asilimia 31.1.
"Tunaamini kwa uhakika kwamba bado kuna maeneo ambako tuna wafuasi wengi...Tuna uhakika kwa ripoti zinazotufikia, UP itaongoza," Boakai aliliambia shirika la Reuters baada ya matokeo kutangazwa Ijumaa.
Mwanasheria Charles Brumskine, anashika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia asilimia 9.3 ya kura zilizohesabiwa.
Ikiwa mchuano utaendelea hivi, upo uwezekano uchaguzi wa marudio kati ya vinara wawili wa mwanzo utaamua mtu wa kurithi Ikulu inayoachwa na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Ellen Johnson Sirleaf anayemaliza muda wake.
Kwa mujibu wa NEC matokeo ya mwisho yaliyohakikiwa kutokana na uchaguzi uliofanyika Oktoba 10 yatatangazwa Oktoba 25, ingawa kwa ujumlishaji huu mshindi atajulikana hata kabla.
Weah, aliyewahi kutamba alipozichezea klabu za Paris Saint-Germain ya Ufaransa na AC Milan ya Italia na ambaye alitangazwa Mwanasoka Bora wa Dunia wa FIFA mwaka 1995, alishika nafasi ya pili nyuma ya Johnson Sirleaf mwaka 2005 aliyemaliza miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha vifo vya maelfu ya raia.
Kuanzia mwaka 2014 amekuwa Seneta kupitia chama cha upinzani cha Congress for Democratic Change (CDC).
Tags