HUKU joto la mhemuko wa mchezo wa watani wa jadi likizidi kupanda kwa mashabiki wa timu hizo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga,-
Wametamba kuwa mechi hiyo ni nyepesi na kwamba wataendeleza rekodi ya kuwafunga watani zao Simba katika mechi ya ligi hiyo inayotarajiwa kupigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Tangu mwaka 1965, timu hizo zimekutana mara 83 katika mechi za ligi, Yanga ikishinda mara 31, Simba mara 24 huku sare zikiwa 28.
Akizungumza jana jijini, Katibu Mkuu wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa kama ilivyo kwa watani zao, Boniface Mkwasa, alisema kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi huko Morogoro na wanaamini kasi ya kutoa "vichapo" ambayo wameianza kwenye Ligi Kuu itaendelea na hatimaye wapate nafasi ya kukaa kwenye uongozi katika msimamo wa ligi hiyo.
Mkwasa alisema kuwa mchezo huo ni wa kawaida kwao kama zilivyo mechi nyingine za ligi, lakini anawaomba mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuwahi kuingia uwanjani mapema na kusisitiza utulivu kwa wale watakaokosa tiketi ili kuiepusha klabu na adhabu kama wenyeji wa mchezo huo.
"Tumejipanga vizuri, tuko vizuri kila idara, hii ni mechi ya kawaida kwetu kama ambavyo tunajiandaa kucheza na Ndanda, ni mchezo wa kujuana, tunawaomba mashabiki kukata tiketi mapema.
Katibu huyo alisema pia klabu hiyo inaendelea na mchakato wa kuhakikisha wanakamilisha uwanja wao ili maandalizi ya msimu ujao wa ligi hiyo yafanyike kwenye Uwanja wa Kaunda ambao ukimalizika utakuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 30,000.
Mkwasa pia alisema klabu hiyo imeteua Kamati ya Soka ya Wanawake ambayo itaongozwa na Hawa Ghasia kwa ajili ya kuanza mchakato wa kuunda timu ya wanawake itakayojulikana kwa jina la Yanga Princess.
MCHEZAJI BORA KUNEEMEKA
Mchezaji ambaye atang'ara katika mechi hiyo ya Jumamosi atajinyakulia zawadi kutoka Benki ya KCB ambao pia ni wadhamini wenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.
Meneja wa benki hiyo, Edgar Masato, alisema jana kuwa mchezaji huyo ambaye atateuliwa na jopo la ufundi litakalofuatilia mechi hiyo, atazawadiwa kitita cha Sh. 500,000.
"Mechi ya Simba na Yanga ni kubwa na ina mashabiki wengi, ili kuongeza hamasa kwa wachezaji wa pande zote kujituma na kuonyesha soka safi kwa ajili ya timu zao, tumepanga kutoa zawadi hiyo," alisema Masato.