Ali Choki Atoa ya Moyoni Kuhusu Muziki wa Dansi

Ali Choki Atoa ya Moyoni Kuhusu Muziki wa Dansi
MUZIKI wa Dansi, ambao miaka kumi iliyopita ulikuwa ndiyo habari ya mjini katika burudani, hivi sasa unaonekana kupoteza mvuto, kiasi kwamba wengi wanaamini upo njiani kuelekea kaburini, ambako tayari tasnia nyingine, Bongo Movie, inasubiri kufukiwa.
Mmoja wa wanamuziki wa dansi la kizazi kipya, Ali Choki ambaye alikuwepo wakati muziki huo ukishika hatamu na anashuhudia wakati huu mgumu, ni Ally Choki mwenye majina mengi ya kisanii, yakiwamo Kamarade, Mzee wa Farasi, Mzee wa Kijiko, Mzigo na mengine kibao.

Katika mahojiano maalum, Choki anapingana na hisia za kudondoka kwa muziki huo, akisema kinachotokea ni kuwepo kwa kundi la watu wenye uwezo ambao hawataki kuiona dansi ikitamba.

Mkongwe huyo anaamini kuwa baadhi ya vituo vya redio, ambavyo ndivyo vilikuwa chachu kubwa ya kukua kwa muziki huo, vimechangia kuukosesha msisimko kwa kuacha kupiga kama ilivyokuwa ikifanya siku za nyuma.

“Zamani kulikuwa na chati mbalimbali kwenye redio, vipindi kama nani zaidi katika muziki wa dansi, top ten na nyimbo zetu zilipigwa mara kwa mara, nyimbo mpya zilizinduliwa na kufanya kuwa na hamasa kubwa miongoni mwa wanamuziki, lakini angalia hivi sasa.

“Hata hizo nyimbo za dansi zimepangiwa vipindi vya usiku sana, wakati ambao watu wameshachoka wamelala, nani atasikiliza nyimbo usiku mkubwa, hata hao wazee ambao unaweza kusema eti ndiyo muziki wao, wameshalala.

“Dansi bado ipo na ina watu, isipokuwa kuna kundi flani la watu hawaupendi huu muziki, wanatamani utoweke, lakini haitawezekana, utakuwepo tu na utarejea enzi zake, katika hili ni lazima tuwashirikishe wadau, hasa vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni, maudhui ya muziki huu bado ni mazuri,” anasema Choki, ambaye kwa mara nyingine, amerejea African Stars ‘Twanga Pepeta’ baada ya kuwa nje kwa miaka kadhaa.

Anasema tatizo kubwa linaloukabili muziki wa Dansi ni kuondoka kwa kizazi chake katika maeneo muhimu ya redio, televisheni na magazeti na kuwepo kwa wale aliowaita, vijana wa Bongo Fleva.

“Kuna watu wapo katika hizo sehemu hawaujui huu muziki, wao wameikuta Bongo Fleva, ndiyo maana kila redio ina chati za muziki wa kizazi kipya, dansi hawana muda nao, lakini pia kuna hawa mapromota nao, wapo tayari kumlipa msanii mmoja shilingi milioni tano, lakini bendi wanataka kwa laki tano, wakati kundi lina watu wengi, hawa nao wanatakiwa kubadilika.

“Sasa hivi hakuna anayehangaika kutaka kujua bendi gani imetoa wimbo gani mpya, tofauti na zamani, kila bendi ilipotoa wimbo mpya, ulipata ‘airtime’ ya kutosha, hapa kuna tatizo la makusudi ambalo linawezekana kabisa kupatiwa majibu,” anasema.

Juu ya mustakabali wake kimuziki, Choki anasema mkataba wake na bendi hiyo utamalizika mwakani, hivyo huu ni wakati wa yeye kutambua nini kitafuata baada ya hapo.

“Kuna vitu vingi vya kufanya kuelekea kumalizika kwa mkataba wangu, sijajua kama nitarejesha bendi yangu au nitatafuta kazi sehemu nyingine, lakini kuna kitu kinapita akilini mwangu ili nijue cha kufanya,” anasema.

Kuhusu kushuka kwa ushindani wa kimuziki baina ya bendi na bendi kama ilivyokuwa miaka iliyopita, alisema hali hiyo inachangiwa na sababu alizotoa mwanzo, kwani kama ni kwenda na wakati, wapo baadhi ya wanamuziki ambao wanabadilika kulingana na mazingira.

“Muziki wa Dansi ni kama jeans tu, miaka nenda rudi ipo, tumez-aliwa tumeikuta na sasa tunazeeka yenyewe ipo tu, inabadilika staili tu, mara pana, mara nyembamba, inayobana na sasa imekuja kwa staili ya kuchanwa, lakini ipo tu.

“Wanamuziki pamoja na wadau wanatakiwa kubadilika kidogo ili urejee, lakini nina uhakika hautakufa na mimi kama mwanamuziki, nitasimama kuhakikisha dansi inarudi na kutesa kama zamani,” anasema Choki, ambaye licha ya African Stars, amewahi pia kupigia Bendi za Bantu Group, Mchinga Sound, TOT Plus, Double Extra na ile aliyokuwa akiimiliki, Extra Bongo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad