Kama ni kuumbuka, basi walioidhinisha kuzikwa kwa maiti iliyodaiwa kuwa ni ya mtu mzima na mwenye ndevu, wameumbuka; maiti hiyo ni ya Humphrey Makundi, mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Scolastica ya Himo wilayani Moshi.
Hayo yalibainika baada ya kutekelezwa kwa amri ya kufukua maiti hiyo iliyotolewa na Hakimu Idan Mwilapo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na baadaye kufanyiwa uchunguzi. Uchunguzi umebaini kuwa maiti hiyo ni ya mtoto na hakuwa na ndevu.
Amri ya kufukua maiti hiyo ilitolewa baada ya Jamhuri kuwasilisha maombi kupitia kwa Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka ukitaka mwili uliozikwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Novemba 12 kwa kukosa ndugu ufukuliwe. Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani juzi yakiambatanishwa na kiapo cha Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), Doto Mdowe na Mahakama iliridhia ombi hilo.
Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6 na baadaye mwili wake ukaokotwa Mto Ghona, umbali wa mita 300 kutoka shule hiyo.
Kutokana na mwili huo kuharibika, polisi na daktari waliufanyia uchunguzi wa awali na kueleza kuwa haukuwa wa mtoto huyo bali ni wa mtu mzima na kuruhusu halmashauri kuuzika.
Ingawa haielezwi katika shauri hilo ni nani aliyetoa hoja mwili huo ufukuliwe, lakini RCO katika kiapo chake alitaka ufukuliwe ili uchunguzwe kama ni wa Humphery aliyetoweka Novemba 6.
Watu 11 wakamatwa
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah alisema wanawashikilia watu 11, akiwemo mmiliki wa shule hiyo iliyopo mji mdogo wa Himo kwa ajili ya mahojiano.
Kwa mujibu wa Kamanda Issah, ingawa mtoto huyo aliondoka Novemba 6 kutoka shule hiyo iliyozungushiwa ukuta na walinzi na kwenda kusikojulikana, taarifa za kutoweka kwake zilitolewa polisi Novemba 11.
“Mtoto alitoweka shuleni tarehe 6.11.2017 wao wakaendelea na taratibu zao hadi tarehe 10.11.2017 ndio walizifikisha taarifa hizo polisi. Tulianzia uchunguzi papo hapo,” alisema.
“Katika hatua za awali za uchunguzi tulimkamata mmiliki wa shule kwa usalama wake kwa sababu wazazi tayari walikuwa wanamtuhumu kuhusika na kifo cha mtoto wao.”
Kamanda Issah alisema wakati wakiendelea na uchunguzi, walipata taarifa kuwa kuna mwili wa mtu uliokotwa Novemba 7 na ukahifadhiwa Hospitali ya Mawenzi hadi Novemba 12 ukazikwa.
“Baada ya kupata taarifa ndipo tukaomba kibali cha kufukua huo mwili na wakati unafukuliwa wazazi walikuwepo. Nawahakikishia haki ya huyu mtoto haitapotea,” alisema.
Kamanda Issah hakutaka kuzungumzia kwa undani kuhusu kile kilichobainika katika uchunguzi huo, lakini alisema umefikia asilimia 50.
“Tunataka kujua ilikuwaje mwanafunzi akatoka shuleni na shule ina geti na ina walinzi. Hapo nje kuna mama lishe,” alisema kamanda huyo.
“Niwaonye wamiliki wa shule, wasimamie vizuri maisha ya wanafunzi.”
Mwili ulivyotambuliwa
Watu walioshuhudia ufukuaji wa mwili huo katika makaburi ya Karanga mjini Moshi juzi saa 8:30 mchana, walilieleza gazeti hili kuwa baba mzazi wa mtoto huyo, Jackson Makundi aliishiwa nguvu na kuanguka.
Taarifa zinasema kabla ya ufukuaji kuanza, maofisa wa polisi walimuuliza mzazi huyo ataje alama zitakazomfanya amtambue kuwa huyo ni mwanaye naye alitoa alama mbili ambazo ni jino moja kukatika nusu na kidole kimoja cha mkononi kuwa na kucha iliyong’oka, alama ambazo zilionekana.
“Baada ya mwili kufukuliwa na baba na ndugu wengine kutambua alama alizozisema, yule baba aliishiwa nguvu na kukaa chini ikabidi aondolewe eneo lile,” alisema mmoja wa walioshuhudia tukio hilo.
Kwa mujibu wa mtu aliyeshuhudia uchunguzi huo, mwili wa mtoto huyo umekutwa na jeraha kwenye fuvu la kichwa ikiashiria alipigwa na kitu kizito kichwani.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Alichosema baba mzazi
Jackson Makundi, baba mzazi wa mtoto huyo amedai kuna mchezo uliofanywa baina ya uongozi wa shule na polisi wa Himo ili kuficha ukweli kuhusu ukatili aliofanyiwa mtoto wake.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, baba huyo alidai alipewa taarifa za kupotea mwanawe Novemba 8, ikiwa ni siku mbili baada ya kudaiwa ametoweka shuleni katika mazingira ya kutatanisha.
Makundi alidai taarifa ambazo baadhi ya walimu wanazitoa kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo zinatofautiana na taarifa za wanafunzi.
“Baada ya mwili kufukuliwa nilijiridhisha kwa asilimia 100 kuwa mtoto ni wangu kutokana na kwamba vichwa vyetu vinafanana na nyuso zetu,” alisema.
Alidai taarifa alizozipata kutoka kwa wanafunzi wenzake ni kwamba mtoto wake aliondoka shuleni akiwa amevaa bukta, fulana na soksi.
Makundi amehoji iweje mwanafunzi atoweke shule halafu apewe taarifa baada ya siku mbili, wakati shule hiyo ina ulinzi na utaratibu mkali wa kuingia na kutoka.
“Ninaamini na dhamira ya moyo wangu inanituma kuamini uongozi wa shule na polisi wa kituo cha Himo wana jambo wanalificha kuhusu kifo cha mtoto wangu,” alisema.
Hata hivyo, alimpongeza Kamanda Issah na wasaidizi wake kwa namna wanavyompa ushirikiano katika uchunguzi, akiamini kila kitu kitajulikana.
Maswali kuhusu uchunguzi
Tangu kufukuliwa kwa mwili huo na kubainika ni wa Humphrey, kumeibuka maswali kuhusu namna polisi na daktari wa Hospitali ya Mawenzi walivyoruhusu mwili uzikwe.
Taarifa kutoka eneo ambalo mwili huo uliokotwa zilidai polisi hawakupiga picha pande zote za mwili huo ili iwe rahisi kwa mtu yeyote kuutambua.
Imeelezwa polisi walitafuta picha na kupata kutoka kwa mwananchi aliyezipiga kwa kutumia simu zikionyesha mwili huo ukiwa umelala kifudifudi.
“Ndiyo maana ukitazama polisi siku mwili unaokotwa wana picha moja ya marehemu akiwa amelala kifudifudi. Huu ndio utaratibu wa kiuchunguzi?” Alihoji mmoja wa wajumbe wa Serikali ya Mji wa Himo.
Swali jingine ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakihoji ni jinsi polisi na daktari wa Hospitali ya Mawenzi walivyoruhusu mwili huo uzikwe wakidai ni wa mtu mzima mwenye ndevu wakati ni wa mtoto.
Pia, wanahoji ilikuwaje mwanafunzi atoweke shuleni tangu Novemba 6, lakini taarifa za kutoweka kwake zikafikishwa polisi siku tano baadaye.
Swali jingine ni kwanini polisi waliofika mahali sehemu ulipookotwa mwili huo, hawakuchukua sampuli za vipimo vya vinasaba (DNA) ili atakapojitokeza ndugu, waweze kuoanisha.
Utaratibu unataka maiti isiyojulikana inapookotwa yatolewe matangazo katika maeneo yote ya jirani, lakini katika tukio hilo, mwili ulichukuliwa na kupelekwa hospitali na baadaye kuzikwa.
By Daniel Mjema na Janeth Joseph, mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Kwa tz itaisha tu hila inatia uchungu
ReplyDelete