Klabu ya soka ya Arsenal imethibitisha kumteua Raúl Sanllehí kuwa mkuu wa michezo na mahusiano, ambapo ataanza kazi rasmi mwezi Februari.
Uteuzi wa Sanllehi ni sehemu ya maboresho ambayo klabu hiyo inayafanya, kitendo ambacho kinatafsiriwa na wachambuzi wa soka kama ni kuelekea zama za mwisho za kocha mkongwe Mfaransa Arsene Wenger.
Sanllehí amewahi kuwa mkurugenzi wa michezo wa Barcelona ambapo alihudumu klabuni hapo kwa miaka 14 akianza na majukumu ya mahusiano kabla ya kuwa mkurungezi wa michezo.
Moja ya majukumu ambayo yametajwa kuwa yatasimamiwa na Sanllehi ni usajili ambapo atashauriana na kocha Wenger lakini maamuzi ya mwisho yatatoka kwake pamoja na mtendaji mkuu wa klabu hiyo Ivan Gazidis na mjumbe wa kamati ya usajili Huss Fahmy. Mbali na usajili Sanllehi ataiwakilisha Arsenal kwenye mahusiano ya ndani na kimataifa.
Hivi karibuni Arsenal imemteua Sven Mislintat kutoka Borussia Dortmund kuwa Skauti mkuu wa klabu akichukua nafasi ya Steve Rowley ambaye ameitumikia klabu hiyo kwa miaka 21.