Chadema Yaonya Msafara Nyalandu Kupigwa Mabomu

Chadema Yaonya Msafara Nyalandu Kupigwa Mabomu
SIKU moja baada ya msafara wa viongozi wake wakuu kupigwa mabomu na Jeshi la Polisi jijini Mwanza, Chadema kimeonya kuwa tabia hiyo ikiachwa iendelee bila kukemewa, itakuwa na athari kubwa kwa nchi.

Juzi, polisi jijini Mwanza walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wanasindikiza msafara wa viongozi wakuu waliokuwa na mwanachama mpya Lazaro Nyalandu.

Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii kukabidhiwa rasmi kadi ya uanachama wa Chadema kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Mhandu wilayani Nyamagana jijini humo.

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana akiwa jijini Arusha, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema chama chake kinasikitishwa na matukio ya viongozi na wafuasi wake kupigwa mabomu na Jeshi la Polisi bila sababu za msingi.

Alisema tabia hiyo inapaswa kukemewa kwa maslahi ya ustawi wa jamii na ukuaji wa demokrasia nchini.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema wanasikitishwa na tabia hiyo inayoendelea kujengeka ya vyombo vya usalama kusababisha vurugu kwenye mikusanyiko ya Chadema.

Alidai viongozi wanapopita njiani na wananchi kuwasimamisha ili wawasalimie ni kitu cha kawaida kwa kuwa hata misafara ya viongozi wakuu wa nchi imekuwa ikisimamishwa na wananchi barabarani na wamezungumza nao na kusikiliza kero zao.

Alisema hali imekuwa tofauti kwenye mikusanyiko na misafara ya Chadema ambayo wananchi wamekuwa wakikumbana na kipigo hata kama hawajasababisha jambo lolote linalokiuka sheria na taratibu za nchi.

"Jana (juzi) Mwanza walipiga mabomu," Mbowe alisema, "wamepiga mabomu kwa Mheshimiwa (John) Mnyika (Kibamba, Dar es Salaam), wamepiga mabomu Momba (jimboni kwa David Silinde - Chadema).

"Wame-arrest' (wamekamata) vijana wetu, wamepiga vijana wetu, wanawaumiza bila sababu, wameharibu magari ya chama. Hili jambo si la kulifumbia macho. Ni tabia ambayo imezidi kujengeka miongoni mwa vyombo vya dola."

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alisema viongozi lazima waikatae kwa kuwa inaweza kuipeleka nchi kubaya.

"Sasa tunasema siasa zifanyike kistaarabu, unaposhangiliwa wewe na wenzako wanaweza kushangiliwa vilevile," Mbowe alisema na kueleza zaidi:

"Hali kadhalika, unapozomewa wewe, na wenzako wanaweza kuzomewa vilevile. Sasa haiwezekani Misafara ya CCM ikisimamishwa
na wananchi wakiwapongeza, polisi wanalinda lakini Chadema wakisimamishwa na wananchi kutaka kusalimiana na viongozi, wanapigwa mabomu bila sababu ya msingi.

"Unapiga mabomu wananchi ambao wamekusanyika kwenye mkutano, hawana ugomvi na mtu. Sasa kushangilia kwao vyama vya upinzani linakuwa tatizo?"

Mbowe alidai kuwa CCM wanapaswa kutambua kwamba hawawezi kubadili fikra na kugeuza mawazo ya wananchi ambao wameamua kuunga mkono Chadema na kuiamini kwa kuwapiga mabomu na kuwaumiza viongozi wake.

"Nawaambia tu CCM kwamba huu mchezo wa siasa wawaache wananchi waucheze, wawaache wananchi waamue, ndiyo maana ya 'freedom' (uhuru), ndiyo maana ya uhuru, ndiyo maana ya demokrasia," alisema.

"Serikali au CCM haviwezi kuanza kuwaona wananchi kama wabaya pale wanapoanza kuviunga mkono vyama vya upinzani.

"Jana (juzi) Mwanza polisi wametumia nguvu kubwa ambayo haikuwa na sababu, wamepiga wananchi mabomu, msafara wetu ulipigwa mabomu. Mimi mwenyewe nilikuwapo, Mheshimiwa Nyalandu nilikuwa naye gari moja na Mheshimiwa (Godbless) Lema
(Mbunge wa Arusha Mjini).

"Tulipigwa mabomu bila sababu ya msingi. Wananchi wakaanza kutawanywa, polisi wengine wakaanza kupiga virungu wananchi, jambo hili ni baya na litapelekea uhusiano mbaya na kujenga chuki katika jamii."

Mbowe alisema wanaendelea na kampeni za uchaguzi huo mdogo wakiwa na Nyalandu mkoani Arusha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad