Dk Kigwangalla Afuta Vibali Vipya vya Uwindaji Vilivyokuwa Vianze Januari 2018

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla Oktoba 22,2017 alitoa kauli ya kufuta vibali vyote vya uwindaji kwa kampuni na kutoa siku 60 kwa watendaji ili waratibu mchakato upya utakaowezesha vitalu kugawiwa kwa mnada.


Jana Jumatatu Novemba 6,2017 kupitia mitandao ya kijamii Dk Kigwangalla ametoa andiko linalosomeka ifuatavyo:

KWA UFUPI: Kuhusu Vitalu vya Uwindaji

Na Dkt. Hamisi Kigwangalla

Nimefuta vibali vipya vya uwindaji vilivyokuwa vianze Januari 2018. Nitatangaza upya mchakato mpya wa ugawaji vitalu kwa njia ya mnada - sasa hivi wataalamu wetu wanatengeneza utaratibu utakaotumika kuuza vitalu kwa njia ya mnada wa wazi. Pia, tunarekebisha sheria na kanuni kabla ya kuanza mchakato mpya. Hivyo waliokuwa na vibali vya zamani, uhai wake unaisha Disemba 31.

Kimsingi mchakato wa vibali nilivyovifuta haukuwa halali kisheria, ulijaa rushwa na upendeleo na haukuwa wa kimkakati, sababu Mpango wa Taifa wa miaka mitano (2016 - 2021) unaelekeza twende kwenye njia ya mnada, BRN inaelekeza twende kwenye njia ya mnada!

Wataalamu walifaidika na utaratibu wa zamani - hawa walifanya tathmini ya nani 'ameendesha kitalu vizuri, nani ameendesha vibaya, hivyo wapendekeze kwa waziri nani apate nani akose' (hapa kulikuwa na watu walitoa rushwa mapema kabisa ili kujihakikishia wanapata vitalu; wanasiasa hususan Mawaziri waliokalia hiki kiti zamani nao walifaidika na utaratibu huu wa zamani (uliweka mazingira rahisi ya kuamua nani apate nani akose, na maamuzi haya yalikuwa kwenye kichwa cha Waziri pekee - hapo mazingira ya rushwa na upendeleo yalikuwa rahisi kabisa), wafanyabiashara na wawekezaji kwenye sekta hii ya utalii wa uwindaji walikuwa wafaidika wakubwa sababu walitupunja mapato ya ushuru (nchi zingine kitalu kidogo tu kiliuzwa mpaka Dola 2,000,000, sisi tuliambulia Dola 60,000 tu.

Wanasiasa na watu wajanja wanaojiita wazawa, ambao hata hawana weledi wala uwezo wa kuwinda, walikuwa wakichukua vitalu (kwa ushawishi wao kwa Waziri) kisha wanakikodisha kwa waendeshaji wa nje. Wengi walidai pango la hadi Dola 300,000 kwa mwaka, huku wao wakilipa serikalini Dola 60,000 tu.

Utaratibu huu wa zamani uko kinyume kabisa na tafiti mbalimbali zilizofanyika miaka ya mwishoni mwa tisini na mwanzoni mwa miaka ya 2000. Leo zaidi ya miaka 20 hakuna aliyethubutu kubadilisha utaratibu. Sababu kubwa ni syndicate ya wanufaika, tena wachache wale wale tu. Ikawa maeneo haya wamejimilikisha kama yao milele.

Uamuzi wangu kuufuta utaratibu huu ni dhahiri umewaudhi wengi na najua watanishambulia sana. Naombeni dua zenu. Tanzania ilihitaji mmoja wetu afike mahali aseme 'sasa basi' na tutake tusitake iwe hivyo, Rais Magufuli amejitoa, Mimi namuunga mkono kwa 'vitendo', nasema sasa basi! Nitamsaidia kazi hii kwa uaminifu, uadilifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu. Si amenipa kazi, kazi nitafanya! Dua zenu tu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad