Ally Khalfani Ngasa ambaye ni kaka wa mchezaji wa Mbeya City Mrisho Ngasa amesema mdogoake alitakiwa kuvaa moyo wa uvumilivu kama Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ili afanikiwe katika soka la kimataifa.
Ally Ngasa amesema nafasi ambayo aliipata mdogoake kama angekuwa mvumilivu huenda angekuwa mbali badala ya uamuzi wake wa kuvunja mkataba na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
“Hayakuwa maamuzi sahihi, hata Samatta alivyokwenda TP Mazembe hakuanza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, alivumilia badae akawa anaingia kipindi cha pili lakini badae akawa anategemewa na timu. Ngasa alitakiwa kuvumilia kama walivyovumilia Samatta na Ulimwengu.”
“Ngasa alivunja mkataba ili awe huru kwenda timu nyingine kwa sababu timu aliyokuwepo (Free State Stars) alikuwa hapati nafasi ya kucheza, hiyo ndio sababu aliyomwambia mzee.”
“Mpira siku zote ni mchezo wa uvumilivu kwa sababu uwezo wake ulikuwa ni mkubwa asingekosa timu nje. Sasa hivi yupo Mbeya City uwezo wake umepungua sio kama zamani halafu hasikiki kama alivyokuwa Yanga, Azam na Simba.”
Kaka yake Ngasa bado anaamini mdogoake anaweza kutoka tena kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa sababu bado umri wake unamruhusu.
“Umri bado unamruhusu kwa sababu hata miaka 30 bado hajafikisha akijipanga vizuri akarudi kwenye kiwango chake cha zamani anaweza kutoka tena kucheza nje ya nchi.”