Mbunge wa Jimbo la Kawe Halima James Mdee (CHADEMA) amesema hoja inayoenezwa kwamba upinzani wameishiwa sera hivyo kufanya tukio la Mbunge mwenzao (Tundu Lissu) kama agenda kuu ni hoja nyepesi sana kwa suala zito kwani wao kama chama hawawezi
kunyamaza kimya kwa tukio ambalo lingemtoa uhai kiongozi huyo.
Mh. Mdee ametoa jibu hilo wakati akifanya mahojiano na EATV website na kusema kwamba kama Chama ambacho Mbunge wao amepata matatizo katika eneo ambalo linaaminika liko salama kamwe hawawezi kukaa kimya na kuongeza kwamba hoja ya wao kutembelea kiki hiyo iishe, na vyombo vya usalama wanapaswa kuhakikisha wanawakamata waliofanya shambulio hilo
"Hatuwezi kukaa kimya kwa matukio yanayotokea, huu siyo utamaduni wenu. Siyo utamaduni wetu watu kupotea bila jeshi la polisi kutoa taarifa inayoeleweka, viongozi kutolewa silaha hadharani na watu ambao wanaaminika wanajulikana lakini hatujaona wakichukuliwa hatua. Mbunge kupigwa risasi maeneo yenye CCTV kamera na waliofanya tukio hilo kutokamatwa, Wananchi kuchanga fedha kwa ajili ya maafa na kisha kutumiwa kwa kazi nyingine na serikali au ni kiki ipi ambayo tunaitumia au kiki ni nini wakati tunakemea mambo yanayohatarisha ulinzi na Usalama? " Mh. Mdee.
Mbunge Mdee amesema kwamba kama ni sera chama chao bado kina sera nyingi ambazo wanaendelea kuzitekeleza kuanzia zile ambazo waliziahidi wakati wa uchaguzi na kwamba kama chama hawawezi kushindwa kuwa na sera lakini ni lazima wakemee mambo ambayo awali hayakuwahi kuzoeleka kuonekana nchini.
Akigusia suala la Mbunge wa Singida Mashariki kupigwa risasi Mdee amesema "Lissu alikuwa ni mtu wa Kufa ila kwa kudra za Mungu ameushinda mauti ndiyo maana tunapaza sauti kwa tukio lililotokea kwani hatufahamu tukikaa kimya nani mwingine atafuata hivyo niwashauri watu wasitoe majibu mepesi kwenye hoja nzito".