Hizi ndizo Sababu za Mke wa Mugabe Kuchukiwa

Wakati mwisho wa utawala wa miaka 37 wa mume wake Aliyekuwa Rais Robart Mugabe wa Zimbabwe ukiwa wa aibu, sababu tano za wananchi wa taifa hilo kumchukia Grace Mugabe zimeanikwa.

Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ya kijamii na magazeti ya nchi hiyo, Grace Mugabe alisababisha watu kumchukia kutokana na tabia yake ya kupenda kufanya manunuzi ya gharama ambayo yalisababisha kupewa jina la utani la First Shopper, badala ya first Lady. Manunuzi hayo yanadhaniwa kutumia fedha za umma.

Sababu nyingine inayotajwa kumfanya achukiwe ni ubabe, ambao aliounyesha katika matukio mbalimbali ya hadhara, alipokuwa akiongozana na mume wake katika shughuli za kisiasa. Katika hafla nyingi, Grace aliweza kuwafokea maofisa wa serikali hadharani na kumfanya kuogopwa kupita kiasi.

Licha ya sifa hizo, pia mwanamke huyo aliyezaa na Mugabe akiwa bado kwenye ndoa yake, anadaiwa kuwa mgomvi, kwani mara kadhaa ameripotiwa kuwapiga watu, wakiwemo waandishi wa habari na watu wa kawaida, kama ilivyokuwa mapema mwaka huu, alipompiga na kumuumiza msichana mmoja wa miaka 20 nchini Afrika Kusini, baada ya kumkuta akiwa na watoto wake wa kiume hotelini.

Jambo lingine lililomfanya kuchukiwa na wananchi wengi wa nchi hiyo ni tamaa yake ya madaraka, kwani licha ya kuwa kiongozi wa Jumuia ya wanawake wa Zanu PF, pia kwa nyakati tofauti alionyesha kutamani kuchukua nafasi ya mume wake, kitu kilichofanya wananchi wake kuona kama nchi inataka kuendeshwa kifamilia.

Inadaiwa hata kuondolewa kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangangwa, kulifanywa na Mugabe kwa shinikizo lake. Kitu kingine kinachowaudhi wananchi wa nchi hiyo ambayo fedha yake haina thamani kutokana na vikwazo kutoka nchi za Magharibi, ni kitendo chake cha kukosa heshima za kike, hasa tabia yake ya kuropoka hovyo katika hafla mbalimbali zinazohitaji staha kwa wanawake.

Hadi wakati gazeti hili likienda mtaani, bado haikujulikana alipo mwanamke huyo mzaliwa wa Afrika Kusini, baadhi ya habari zikisema amekimbilia Namibia, lakini wengine wakisema amedhibitiwa nchini Zimbabwe
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad