Inspekta Jenerali was Polisi IGP Simon Sirro akipokea salaam ya heshima kutoka kwa askari was Mkoa wa Pwani mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ziara ya kikazi. IGP amewataka askari wa Mkoa wa Pwani kutoa huduma bora na kuendelea kuimarisha nidhamu ili wananchi waendelee kuwa na imani na Jeshi la Polisi.
Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Simon Sirro akikagua baadhi ya askari wa Mkoa wa Pwani mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Sirro akikagua baadhi askari wa Mkoa wa Pwani mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Sirro akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng, Evaristi Ndikilo alipowasili Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
IKIWA ni siku chache baada ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza Bandarini ya dar es Salaam na kukagua magari ya polisi ambayo yaliingizwa nchini mwaka 2015, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amesema kwamba magari mawili atayapeleka mkoani Pwani.
Rais Magufuli alibaini ukwepo kwa magari zaidi ya 50 yakiwa bado yanaendelea kubaki eneo la bandari huku ikielezwa kuwa ni ya Jeshi la Polisi na mengine ni ya Ofisi ya Rais ambapo alimwagiza IGP kuhakikisha anayakagua magari hayo na kuyatoa bandarini ili yakafanye kazi iliyokusudiwa.
“Kwa nini magari yanakuja hapa yanakaa miaka 10, wakati sheria inasema ni siku 21? alihoji Rais Magufuli.
Baada ya siku moja Sirro alitembelea bandarini hapo kuyakagua magari hayo na jana akiwa Kibaha, Pwani alisema anatarajia kutoa magari mawili ya polisi Mkoa wa Pwani ili kupunguza changamoto ya uhaba wa vyombo vya usafiri kwa askari.
“Hayo magari ni ya Jeshi la Polisi na mawili kati ya hayo natarajia kuwapa polisi Mkoa wa Pwani,” alifafanua alipokuwa kwenye ziara ya kikazi.
Sirro alisema kuimarika kwa hali ya usalama kwenye maeneo ya Kibiti, Ikwiriri na Rufiji kumetokana na ushirikiano uliofanyika baina ya jeshi hilo na wananchi wenye nia njema.
“Silaha zote ambazo wahalifu walikuwa wamezipora kwenye matukio mbalimbali wakati hali ikiwa mbaya kule Kibiti, tayari tumeshazipata zote na hali imeshaimarika vizuri hivyo napenda kuwaambia wananchi wote hivi sasa hali ni shwari,” alisema.
Aidha IGP aliwataka askari wa Mkoa wa Pwani kutoa huduma bora na kuendelea kuimarisha nidhamu ili wananchi waendelee kuwa na imani na Jeshi la Polisi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo aliishukuru Serikali kwa kuanzisha Mkoa wa kipolisi Rufiji akisema hali hiyo imesaidia kuimarisha usalama ndani ya Mkoa wa Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna alisema ziara hiyo imeamsha ari ya utendaji kazi kwa askari wake na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa kwake.